• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:24 PM
VALENTINE OBARA: ‘Tosha’ ya Joho si hakikisho ya mteremko uchaguzini

VALENTINE OBARA: ‘Tosha’ ya Joho si hakikisho ya mteremko uchaguzini

Na VALENTINE OBARA

WANASIASA wanaotafuta nafasi ya ugavana katika Kaunti ya Mombasa, wamefanya kampeni tele kujitafutia umaarufu mapema mwaka huu.

Wakati kampeni hizo zinapoendelea, suala moja kuu ambalo limejitokeza ni mdahalo kwamba atakayepata uungwaji mkono wa Gavana Hassan Joho atakuwa na nafasi nzuri ya kushinda wadhifa huo katika uchaguzi ujao.Ijapokuwa Bw Joho ameashiria kuwa huenda atamuunga mkono Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir kujaza nafasi hiyo kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, kuna wadadisi ambao wangali wanamsubiri ajitokeze kwa ukakamavu zaidi kutangaza msimamo wake halisi kuhusu urithi wake.

Bw Nassir anatafuta tikiti ya Chama cha ODM kuwania wadhifa huo, na yuko katika kinyang’anyiro hicho dhidi ya mfanyabiashara Suleiman Shahbal na Naibu Gavana, Dkt William Kingi.Mmoja wa wanachama hao wa ODM ndiye anatarajiwa kupata ‘tosha’ halisi ya Joho kuelekea kwa uchaguzi ujao, ikizingatiwa kuwa gavana huyo pia ni naibu kiongozi wa chama hicho.

Kimataifa, imekuwa desturi kwa wanasiasa wanaopanga kuwania kurithi viti vya kisiasa ambavyo vinaelekea kubaki wazi kutafuta uungwaji mkono kwa kiongozi yule ambaye anakamilisha hatamu yake ya uongozi kisheria.Hili hutendeka kwa vile inaaminika kiongozi ambaye amefanikiwa kukaa mamlakani kwa muda wake wote anaokubaliwa kisheria, ana siri na mikakati ambayo inaweza kuwa ya manufaa kwa yeyote anayetaka kurithi kiti hicho.

Humu nchini, mwaka ujao itakuwa ni mara ya kwanza kwa cheo cha ugavana kushuhudia siasa za urithi kwani hii ni mara ya kwanza tangu katiba iliyoleta ugatuzi kupitishwa, kwa magavana wa baadhi ya kaunti zetu kutumikia uongozi kwa vipindi viwili vya miaka kumi.

Lakini, je, uungwaji mkono na kiongozi aina hiyo humaanisha kuwa mgombeaji atapata mteremko uchaguzini? La, hasha!Kumekuwa na matukio humu nchini na vile vile katika mataifa mengi ya kigeni ambapo wananchi hukataa kufuata upande wa kiongozi anayeondoka mamlakani.

Nchini Kenya, mfano bora wa mwelekeo aina hii ulishuhudiwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2002, ambapo aliyekuwa rais Daniel arap Moi alikuwa anastaafu.Wakati huo, Moi alitaka Uhuru Kenyatta ndiye awe mrithi wake, lakini hilo likaambulia patupu kwani wananchi walisimama na Mwai Kibaki.

Kimsingi, kiongozi anayeondoka anaposema ‘fulani tosha’ huwa inaweza ikawa baraka au laana kwa ‘fulani’ huyo.Itakuwa ni baraka kama wapigakura watakuwa wamefurahia uongozi wa yule anayeondoka na wana imani kuwa mrithi anayesimama naye ataendeleza mafanikio hayo.

Kwa upande mwingine, laana itatokea kama wapigakura watahisi hawakufaidika katika utawala unaoondoka.\, na wanatamani mabadiliko.Haya ni kando na masuala mengine ambayo huathiri matokeo ya uchaguzi humu nchini kama vile umaarufu wa chama na mgombeaji binafsi, uaminifu katika usimamizi wa uchaguzi, miongoni mwa masuala mengine.

You can share this post!

Zaha kutegemewa na Ivory Coast kwenye AFCON 2022 nchini...

KINYUA BIN KINGORI: Wakenya wasipuuze chanjo ya corona...

T L