• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
MUTUA MUEMA: Tusherehekeni Krismasi ndio, lakini tusivuke mipaka iliyopo

MUTUA MUEMA: Tusherehekeni Krismasi ndio, lakini tusivuke mipaka iliyopo

Na MUTUA MUEMA

LEO ni Krismasi, sikukuu ambayo inasherehekewa na watu wengi zaidi duniani. Wengi wanakula vitamu, vinono na kuvalia maridadi ajabu!La kushangaza, au hata kuchekesha ni kwamba, watu wengi huisherehekea iwe yawe tu, bila kuwa na ufahamu wa ndani kwa ndani kuihusu sikukuu yenyewe.

Wapo pia wanaoisherehekea bila kujua, hasa kwa kuwa inatoa fursa safi kwa watu kufanya biashara, lakini ukiwaambia wanaisherehekea watakanusha.Kimsingi, hii ni sikukuu ya kidini ambapo Wakristo kote duniani husherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Kuna mjadala kuhusu siku hasa aliyozaliwa, baadhi ya watu wakishikilkia kuwa si Desemba 25, lakini nadhani hoja hapa ni kuzaliwa, si siku aliyozaliwa.Kinachonipendeza zaidi kuihusu ni kwamba imetokea kuwa sikukuu ya kuwaunganisha watu kwa njia kadha.

Mathalan, wafanyabiashara ambao si Wakristo na wasiotaka kuisherehekea kamwe hujipata wakipunguaa bei za bidhaa ili Wakristo wamudu kuwanunulia wenzao zawadi.Ni kwa mintaarafu hii ambapo ukitembea jijini kwenye maduka ya Wahindi utapata Miti ya Krismasi na mapambo mengineyo yanayohusiana na sikukuu hiyo.

Muhimu ni kuuza tu, na ndiyo maana utakuta kuwa, ziada ya mapambo ya Krismasi, yapo pia yanayokutangazia kufika kwa mwaka ujao katika muda wa wiki moja. Muuzaji hajali pesa zinatoka mikononi mwa Mkristo, Mhindi, Mwislamu au kafiri wa kutupwa.

Laiti tungalikuwa na uwezo wa kupuuza tofauti zetu za kidini hivyo, dunia ingekuwa mahali bora pa kuishi. Laiti tungaliweza kushiriki sherehe za watu bila kushinikizwa kubadili imani zetu wala kuhofia kwamba tutasingiziwa kufuru na walio wa imani zetu, tungalikuwa na furaha zaidi.

Nimetokea kupendezwa jinsi watu wa Afrika Magharibi husherehekea sikukuu za dini zote bila kujali watachukuliwa vipi. Waislamu hurembesha nyumba zao kwa Miti ya Krismasi, sikwambii huimba hata nyimbo za Krismasi, lakini hawabadili imani yao kwa kufanya hivyo.

Wakristo nao huvalia kama Waislamu, kina dada wakapaka hina na kutia uturi kabla ya kuungana na Waislamu kusherehekea Sikukuu za Idd. Hawabadili imani yao, wala hawasingiziwi ukafiri na yeyote kwa kuwa hizo ni sherehe tu, muhimu ni uhusiano binafsi wa mtu na Mungu wake.

Kitu ambacho si sawa wakati wa sherehe za imani zote ni watu kushiriki ya hovyo, wakahatarisha maisha yao, wakafuja pesa na kualika umaskini mwezi mkavu wa Januari! Kulewa chakari na kujiendea haja, kisha mtu akapigwa picha na wapiti-njia zikatokea mtandani, eti kwa ajili ya Krismasi, ndiko kupotoka hasa. Kila kitu kifanywe kwa kiasi. [email protected]

  • Tags

You can share this post!

Sababu za Lamu kuibuka ‘ngome ya kijeshi’ Pwani

WANDERI KAMAU: Ni ukiukaji mkubwa wa katiba kudhalilisha...

T L