• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 10:55 AM
Sababu za Lamu kuibuka ‘ngome ya kijeshi’ Pwani

Sababu za Lamu kuibuka ‘ngome ya kijeshi’ Pwani

Na KALUME KAZUNGU

KAUNTI ya Lamu inazidi kuibuka kama eneo la Pwani lililo na kambi nyingi za jeshi la kitaifa (KDF) baada ya serikali kuzindua miradi mingine ya kijeshi mwaka huu katika eneo hilo.

Katika mwaka huu, serikali ya kitaifa ikiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta ilipandisha hadhi kambi ya jeshi la wanamaji eneo la Manda-Magogoni.Hafla ya kupandishwa hadhi kwa kambi hiyo ilifanyika Septemba 23 na kuongozwa na Rais Kenyatta.

Kwenye hotuba yake wakati wa hafla hiyo, Rais alisema serikali itafanya kila jitihada kuona kwamba eneo la Lamu lililoko mpakani mwa Kenya na Somalia linalindwa vilivyo kutokana na uvamizi wa magaidi wa Al-Shabaab kutoka nchi hiyo jirani.Rais Kenyatta pia alisisitiza kuwa serikali itaendelea kutunza mipaka yake, hasa ile iliyoko mwenye kaunti ya Lamu na kuona kwamba maendeleo yaliyolengwa na serikali, ikiwemo mradi wa Bandari ya Lamu (Lapsset) yanaafikiwa vilivyo.

“Wakati tukipandisha hadhi kambi ya nevi ya Manda, wananchi wajue kuwa Lamu na Pwani kwa jumla lazima ilindwe vilivyo, ikizingatiwa kuwa haya ndiyo maeneo yaliyo na njia za kibiashara,ikiwemo meli na mengineyo. Jamii ya hapa ishirikiane na serikali kuona kwamba usalama unadhibitiwa kwa manufaa ya nchi na wananchi,” akasema.

Utafiti uliofanywa na Taifa Leo aidha ulibaini kuwa mbali na kambi ya nevi ya Manda, mipango ya serikali kuongeza kambi za jeshi Lamu imekuwepo kwa muda mrefu.Katika mwaka wa 1985, serikali ilianzisha kambi ya jeshi ya Bar’goni iliyoko msitu wa Boni ili kudhibiti usalama zaidi maeneo ya mpakani mwa Lam una Somalia.

KUFURUSHA MAGAIDI

Mnamo 2015, serikali kuu pia ilizindua oparesheni ya usalama kwenye msitu wa Boni, dhamira kuu ikiwa ni kuwafurusha au kuwamaliza magaidi wa Al-Shabaab wanaoaminika kujificha ndani ya msitu huo mkuu wanaoutumia kama ngome yao kuendeleza mashambulizi na mauaji kwenye sehemu tofauti za Lamu, Pwani na nchini.

Kuzinduliwa kwa oparesheni hiyo aidha kumepelekea makumi ya kambi za jeshi na polisi kubuniwa kwenye sehemu mbalimbali za Lamu.Miongoni mwa kambi hizo ni Baure, Kotile, Milimani, Bodhei, Mangai, Basuba,Kiangwe, Kotile, Sankuri, Kiunga, Ishakani, Ras Kiamboni, Sarira, Hulugho, Sanghailu, miongoni mwa nyingine.

Wakati huo huo, serikali pia inaendeleza mjadala wa kuanzisha kambi nyingine ya jeshi eneo la Witu.Ni mwaka huu ambapo serikali tayari imeweka kwenye gazeti rasmi la serikali tangazo la kutaka kubuni kambi ya jeshi eneo la Witu na Chara/Kipini mpakani mwa Lamu na Tana River.

Karibu ekari 30,000 za ardhi zinalengwa kutwaliwa kufanikisha ujenzi wa kambi hiyo kubwa ya jeshi.Uchunguzi wa Taifa Leo ulibaini kuwa kichocheo kikuu cha serikali kuendeleza uzinduzi wa kambi za jeshi Lamu ni zogo la Al-Shabaab.Lamu ni mojawapo ya maeneo ya nchi ambayo huchukuliwa kama kitovu cha misukosuko ya Al-Shabaab, kwa sababu ya mpaka wa Kenya na Somalia uliozingirwa na msitu mkubwa wa Boni eneo hilo.

Kisa cha kwanza cha utekaji nyara dhidi ya raia wa kigeni kilichotekelezwa na maharamia wanaoaminika kuwa Al-Shabaab kilifanyika Lamu.Kisa hicho ni kile cha Septemba, 2011, ambapo wachumba raia wa Uingereza, David Tebbut na mkewe Judith Debbut walivamiwa usiku na magaidi wa AL-Shabaab wakiwa kwenye fungate yao katika hoteli ya Kiwayu Safari Village, eneo la Lamu Mashariki.

Kwenye uvamizi huo, Bw Tebbut aliuawa ilhali mkewe Judith akitekwa nyara na magaidi hao.Isitoshe, ni mwaka huo huo ambapo mwanamke mtalii, raia wa Ufaransa alitekwa nyara na magaidi wa Al-Shabaab kwenye hoteli moja Lamu.Utovu huo wa usalama uliisukuma serikali kuzindua oparesheni ya Linda Nchi huko Somalia mwaka uliofuatia katika harakati za kukabiliana na Al-Shabaab nchini humo na kumaliza utovu wa usalama kwenye mpaka wa Kenya na Somalia.

Kisa kingine kinachoaminika kilisukuma serikali kuongeza wanajeshi na vitengo vingine vya usalama na kugeuza kaunti ya Lamu kuwa ya kijeshi ni lile tukio la kuvamiwa kwa mji wa Mpeketoni na magaidi wa Al-Shabaab usiku wa Juni 15, 2014.

Shambulizi hilo liliacha zaidi ya wakazi 100, wengi wao wakiwa wanaume kuchinjwa na kuuawa ilhali nyumba na magari vikiunguzwa kwa moto na magaidi hao.

DORIA

Tangu hapo, serikali imekuwa ikiendeleza doria za jeshi na polisi, na hata kubuni kambi za kijeshi na polisi, ikiwemo ile ya Mkunumbi, Maleli na Nyongoro ili kudhibiti usalama eneo hilo.Hata hivyo, kwenye mahojiano na Taifa Leo, Msemaji wa KDF, Bi Esther Wanjiku alisema hatua ya serikali ya kuendelea kubuni kambi za jeshi Lamu isichukuliwe kuwa jambo geni.

Kulingana na Bi Wanjiku, juhudi za kulinda mipaka ya Kenya zimekuwa zikiendelea kila wakati.“Watu wafahamu ya kuwa hakuna geni wanapoona kambi za jeshi zikibuniwa Lamu. Huo ni mpango ambao umekuwa ukiendelea na ni katika harakati za kuhakikisha kuwa maeneoyetu na mpakani nchini yanalindwa na kudhibitiwa vilivyo,” akasema Bi Wanjiku.

Baadhi ya wakazi waliohojiwa na Taifa Leo aidha wamepokea kwa mikono miwili juhudi hizo za serikali kudhibiti usalama wa Lamu kupitia kubuniwa kwa kambi za kijeshi.Mzee wa jamii ya Waboni anayeishi msitu wa Boni, Doza Diza,anasema ni kupitia kuwepo kwa kambi hizo ambapo hali ya kiusalama imeimarika vilivyo Lamu.“Tunashukuru.

Kinyume na awali ambapo tulilazimika kulala msituni kwa kuhofia kushambuliwa na Al-Shabaab, sisi kwa sasa tunalala vijijini bila hofu yoyote. Kambi za jeshi ziko kila mahali na tunahisi tumelindwa ipasavyo,” akasema Bw Doza.Bi Lucy Kimani ambaye ni mfanyabiashara mjini Mpeketoni anasema ni kupitia kuwepo kwa doria za jeshi na kambi za walinda usalama Lamu ambapo imani yao kuhusu usalama wa Lamu imerejea.

“Baada ya shambulizi la Al-Shabaab mjini hapa 2014, wanabiashara wengi, ikiwemo mimi binafsi tuliingiwa na woga. Wengine walihamia maeneo ya mbaliya nchi. Nashukuru kwamba kutokana na bidii za serikali kubuni kambi za jeshi na kuongeza doria barabarani, mijini na kila mahali, imani yetu imerejea. Tunaendeleza biashara kama kawaida,” akasema Bi Kimani.

You can share this post!

Sababu za Ruto kupinga vikali mswada wa vyama

MUTUA MUEMA: Tusherehekeni Krismasi ndio, lakini tusivuke...

T L