• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
DOUGLAS MUTUA: Sudan hatarini kutekwa na jeshi kama Misri

DOUGLAS MUTUA: Sudan hatarini kutekwa na jeshi kama Misri

Na DOUGLAS MUTUA

WAZIRI Mkuu wa Sudan, Bw Abdallah Hamdok, ameingia kwenye kumbukumbu za historia kama kiongozi aliyepinduliwa kisha akarejeshewa mamlaka na waliompindua.

Lakini pia anapaswa kuingia katika kumbukumbu hizohizo kama manusura wa mapinduzi ambaye atapumua kwa mapafu ya kuazima kwa muda mrefu ikiwa jeshi litamruhusu. Nimesema jeshi kumruhusu kwa kuwa mwanajeshi aliyeongoza mapinduzi hayo, Jenerali Abdul Fattah al-Burhan, angalipo na mpaka sasa mambo yanafanywa atakavyo.

Usidanganyike kwamba mkuu huyo wa majeshi ataenda popote baada ya kipindi cha mpito, wala usiwe na hakika kipindi chenyewe kitakamilika kilivyopangwa. Sudan na Misri, kando na kuwa majirani wema, ni kama mapacha. Mambo yao ya kisiasa hutegemeana; Sudan huiga misri hata katika siasa za kimataifa.

Si siri kwamba, Jenerali Al-Burhan anafuata nyayo za somo na msiri wake, Jenerali Abul Fattah al-Sisi aliyepindua serikali ya raia nchini Misri na kujitwika mamlaka! Jenerali Al-Sisi aliwatazama raia na kiherehere chao wakimpindua Hosni Mubarak, wakamchagua Mohammed Mursi wa Muslim Brotherhood kwa makeke, kisha akatwaa mamlaka.

Ili asiitwe dikteta wa kijeshi aliyetwaa mamlaka wa mtutu wa bunduki, Jenerali Al-Sisi alijiuzulu jeshini, akaandaa uchaguzi ambao mwenyewe aliwania na kutawazwa rais. Sasa ni kiongozi wa kiraia eti na dunia nzima inamtambua hivyo; inajitia hamnazo kuhusu maelfu waliouawa na jeshi ili kumweka mamlakani.

Kimsingi, Jenerali Al-Sisi ni mmoja wa wahafidhina wengi jeshini waliompenda Mubarak na sera zake kupindukia hivi kwamba, walisinywa na alivyoondolewa mamlakani na raia. Nina hakika Jenerali Al-Burhan anafuata nyayo hizo na atatimiza malengo yake yote ya kuwa kiongozi wa Sudan kwa vyovyote vile.

Kwa Al-Burhan kumrejeshea mamlaka, Waziri Mkuu Hamdok na mataifa ya magharibi yanayomuunga mkono wanapaswa kuwa na hofu kuu. Jenerali Al-Burhan alishinikizwa na mataifa hayo kufanya hivyo, sikwambii na waandamanaji waliomwagika barabarani kupinga utawala wa jeshi.

Mwanajeshi wa watu alisalimu amri lakini akasalia palepale ili kuendelea kusimamia kipindi cha mpito kabla ya mamlaka yote kurejeshwa mikononi mwa raia. Kumbuka, Jenerali huyo aliipindua serikali ya Bw Hamdok zikisalia siku 30 hivi hadi mwisho wa kipindi cha mpito ambapo wawili hao walisaidiana kutawala nchi.

Sasa wameanza kipindi kingine cha mpito baada ya Bw Hamdok kurejeshwa mamlakani kwa masharti ya Jenerali Al-Burhan. Hivi majuzi tu, Bw Hamdok amechangamka na kuwafuta kazi wakuu wa polisi akiwalaumu kwa kusimamia mauaji ya waandamanaji waliopinga mapinduzi hayo.

Hilo ni kosa la kwanza! Kumbuka polisi waliua watu chini ya utawala wa muda wa Jenerali Al-Burhan, hivyo kuwaadhibu ni kumchokoza kwa mbali tu. Hata kabla ya kupinduliwa, Bw Hamdok akilalamika kuwa misukosuko iliyoukumba utawala wake ilichochewa na wahafidhina jeshini waliokuwa waaminifu kwa Jenerali Omar al-Bashir aliyepinduliwa mnamo 2019.

Mhafidhina wa kwanza katika orodha hiyo si mwingine bali Jenerali Al-Burhan! Ndiye aliyewachochea raia wakaandamana kulitaka jeshi limpindue Bw Hamdok. Nina hakika ameipumbaza dunia tu kwa kumrejesha Bw Hamdok mamlakani; sasa ndio anapanga mikakati ya kuitwaa serikali kikamilifu kwa jinsi itakayohusisha raia.

Akifanikiwa kuwashawishi raia wengi wajitokeze mitaani kupinga utawala wa Bw Hamdok, jeshi litamshinikiza waziri mkuu huyo kung’atuka tena kwa mara ya mwisho. Kisha? Jeshi litashikilia mamlaka kwa muda na kuandaa uchaguzi ambapo Jenerali wa watu atawania urais kama raia baada ya kujiuzulu jeshini.

Na mataifa ya magharibi hayatafanya chochote kwa kuwa mchakato mzima utakuwa umewahusisha raia, ambao ndio wenye mamlaka kamili kwa mujibu wa demokrasia.

[email protected]

You can share this post!

Mibabe kutoana kijasho leo

Serikali yaruhusu wafanyabiashara kuagiza tani 577,000 za...

T L