• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
TAHARIRI: Kazi kwako Ruto, chapa kazi sasa

TAHARIRI: Kazi kwako Ruto, chapa kazi sasa

NA MHARIRI

LEO Kenya inafungua ukurasa mpya – kutoka serikali ya Rais Uhuru Kenyatta anayestaafu leo Jumanne hadi utawala wa Rais William Ruto.

Licha ya kurithi changamoto lukuki kutoka kwa serikali ya Rais Kenyatta, idadi kubwa ya Wakenya wana matarajio tele kwa serikali mpya ya Rais Ruto.

Baadhi ya Wakenya, vilevile, wana hofu.

Wakenya walio na matarajio makubwa kwa Dkt Ruto walishawishiwa na ahadi tele zilizotolewa na muungano wa Kenya Kwanza wakati wa kampeni.

Miongoni mwa ahadi zilizoonekana kuvutia Wakenya ni kupunguzwa kwa bei ya unga kutoka Sh230 kwa sasa hadi Sh90 kwa kilo mbili.

Dkt Ruto pia aliahidi kupunguza bei ya mbolea mara tu baada ya kuapishwa leo uwanjani Kasarani, Nairobi.

Katika kipindi chote cha kampeni za urais, Dkt Ruto alikuwa akiahidi kuinua Wakenya walala hoi kuwa na hela mfukoni.

Kulingana na manifesto ya Kenya Kwanza, hilo litawezekana kwa kuwatengea Wakenya walala hoi kitita cha Sh50 bilioni ambapo watapewa mikopo ya riba nafuu.

Kwa upande mwingine, Wakenya walio na mashaka wanahofia ikiwa Dkt Ruto ataweza kupambana na zimwi la ufisadi, atalinda uhuru wa vyombo vya habari, atafanikiwa kuteremsha gharama ya maisha, kupunguza pengo baina ya mabwanyenye na maskini na kuwezesha mamilioni ya vijana wasio na kazi kupata ajira.

Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 30 ya bajeti ya Kenya huishia katika mifuko ya wachache kupitia ufisadi.

Ufisadi umesababisha Wakenya kukosa huduma muhimu kama vile matibabu, maji safi na salama, mbegu bora, mbolea, chakula kati ya nyinginezo.

Ripoti pia zinaonyesha kuwa ufisadi hupoteza nafasi za ajira 250,000 humu nchini kila mwaka.

Wakenya zaidi ya milioni 5 hawana ajira na idadi hiyo huongezeka kila mwaka.

Japo Dkt Ruto amekuwa ameahidi kupambana na ufisadi, wengi wanatilia shaka ahadi hiyo. Hivyo, Rais Ruto hana budi kuwathibitishia wanaotilia shaka uwezo wake wa kupambana na zimwi la ufisadi kwamba yeye ndiye dawa yao.

Hatua ya kamati andalizi ya uapisho kuzuia baadhi ya vituo vya televisheni kunasa picha na kupeperusha moja kwa moja matukio katika hafla ya kuapisha rais mpya na naibu wake uwanjani Kasarani, Nairobi, imeibua hofu kuwa huenda serikali ya Dkt Ruto ikagandamiza vyombo vya habari.

Rais Ruto hana budi kuviondolea vyombo vya habari hofu hiyo. Vyombo vya habari huchangia pakubwa katika maendeleo ya nchi.

Wakosoaji wa Dkt Ruto pia wanangojea kuona ikiwa ataweza kupunguza deni la kitaifa ambalo sasa limefikia Sh10 trilioni. Deni hilo limeathiri pakubwa uchumi wa nchi.

Hivyo, serikali ya Dkt Ruto ina kibarua kikubwa kuhakikisha kuwa inatimiza matarajio ambayo Wakenya wako nayo kwake.

You can share this post!

Uhuru kukumbukwa kwa sarafu mpya, unifomu ya maafisa polisi

Njama ya Ruto kuteka Pwani kupitia Kingi

T L