• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Njama ya Ruto kuteka Pwani kupitia Kingi

Njama ya Ruto kuteka Pwani kupitia Kingi

KENNEDY KIMANTHI NA ANTHONY KITIMO

USHINDI wa aliyekuwa gavana wa Kilifi Bw Amason Kingi, katika uchaguzi wa uspika katika Bunge la seneti, huenda ni njama ya Dkt William Ruto kuongeza ngome zake za kisiasa, kuhakikisha kuwa ana uungwaji mkono mkubwa katika chaguzi zijazo.

Hatua ya Bw Kingi wa Pwani kupata nafasi ya kuwa spika wa bunge la seneti na mwenzake Moses Wetangula wa eneo la magharibi kushinda uspika wa bunge la kitaifa, iliweka bayana kuwa Dkt Ruto anatarajia kuongeza ngome hizo mbili katika orodha yenye Mlima Kenya na Bonde La Ufa.

Licha ya kuwa na ishara kuwa maeneo ya Magharibi na Pwani yanaegemea upande muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, muungano wa Kenya Kwanza ulitikisa ngome hizo zilizodaiwa kuwa za Bw Raila Odinga, katika kura za Agosti 9.

Kwa muda mrefu, eneo la Pwani limeathirika kisiasa kwa kukosa kiongozi wa asili ya kipwani, anayeungwa mkono na jamii nzima ya Wapwani.

Kulingana na mtaalamu wa masuala ya uongozi Bw Javas Bigambo, Dkt Ruto yuko tayari kupunguza umaarufu wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) katika ukanda wa Pwani.

Miaka miwili kabla ya uchaguzi uliokamilika, Dkt Ruto alifanya safari nyingi katika eneo la Pwani, akishiriki katika michango na hafla nyingine za kisiasa.

“Katika kampeni zake Dkt Ruto alimwonyesha Bw Raila kama kiongozi asiyeweza kutimiza ahadi zake. Kwa kuhakikisha Bw Kingi amekuwa spika amewaonyesha wapwani kuwa ametimiza ahadi zake,” alisema Bw Bigambo.

Hatua hiyo ya kumponda kisiasa Bw Odinga huko pwani pia ilichangiwa pakubwa na hatua ya aliyekuwa gavana wa Nairobi Bw Mike Sonko . Kulingana na Bw Bigambo kapu la kura za ukanda wa pwani la Dkt Ruto katika uchaguzi uliotamatika, lilikuwa nene ikilinganishwa na kura walizopata na Rais anayeondoka Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa mnamo 2017.

Bw Sonko kugura muungano wa Azimio kulikuwa ndondi nzito ya kisiasa kwa Bw Odinga, ikikumbukwa kuwa alikuwa mwandani wa karibu sana wa mgombea huyo wa urais na kinara wa Wiper Bw Kalonzo Musyoka.

“Matokeo ya uchaguzi wa Agosti 9 ni ishara kuwa ODM haina usemi mkubwa Pwani. Kenya kwanza iliweka mikakati kabambe na ikashinda kura. Nina uhakika kuwa Dkt Ruto atatimiza kila ahadi alilowapa Wapwani,” alisema Bw Sonko.

Kulingana na Bw Sonko, Dkt Ruto huenda akaongeza umaarufu katika eneo hilo.

Mchanganuzi wa siasa bw Martin Nyaga anaeleza kuwa miungano ya kitaifa itaathiri pakubwa siasa za Pwani.

“Masuala ya kimaeneo yatachangia sana kubadilika kwa siasa za pwani. Tayri ameshinda kiti cha ugavana ukanda wa Pwani. Wakazi wa Kwale walishaonyesha kuwa hawampendi tena Bw Odinga kama ilivyodhaniwa,” alisema Bw Nyaga.

Licha ya hayo Maseneta Mohamed Faki wa Mombasa, Jones Mwaruma wa Taita Taveta, Juma Boy wa Kwale na Joseph Githuku wa pwani, wameelezea kuwa hawatabadili msimamo wao wa kisiasa kumuunga Bw Odinga.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Kazi kwako Ruto, chapa kazi sasa

Nassir awataka wanaotaka uwaziri kutuma maombi ya kazi

T L