• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 10:10 AM
TAHARIRI: Kuna hakikisho gani kuwa pesa za ziada za NSSF hazitafujwa?

TAHARIRI: Kuna hakikisho gani kuwa pesa za ziada za NSSF hazitafujwa?

NA MHARIRI

BAADA ya mzozo wa miaka kadhaa mahakamani, hatimaye mahakama ya Rufaa imeruhusu Hazina la Malipo ya Uzeeni (NSSF) iongeze kiwango cha pesa za kila mwezi.

Ongezeko jipya kulingana na Sheria ya NSSF ya mwaka 2013, ni mara kumi ya kiwango cha sasa cha pesa ambazo kila mwajiriwa na mwajiri huchangia NSSF.

Mwaka 2001, serikali ilipandisha pesa hizo kutoka Sh160 kwa mwezi hadi Sh200 ambazo kwa sasa watu hukatwa kama malipo yao watakayochukua wakifikisha umri wa miaka 60.

Punde tu alipochukua uongozi, Rais William Ruto alitangaza mipango ya kupandisha pesa hizo.

Alisema si sawa kwa mtu aliyefanya kazi miaka 30 au 40 kuishia na Sh30,000 kama malipo yake anapostaafu.

Kwa sababu hiyo, Dkt Ruto alisema ni heri watu waumie sasa wanapokuwa na nguvu za kupata pesa, na kuweka akiba ya kutosha ya kutumia watakapokuwa hawana mshahara wala njia nyingine ya mapato.

Kauli yake ilijiri wakati kulipokuwa na kesi mahakamani, ambapo Shirikisho la Waajiri (FKE) liliunga msimamo wa mashirika ya Kenya Tea Growers Association na Agricultural Employers’ Association kwamba malipo hayo yasitozwe kwamba kabla ya kushirikisha umma.

Lakini majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa wanasema NSSF iko sahihi kuongeza pesa hizo. Ina maana kwamba kiwango cha chini cha pesa atakazolipa mtu kila mwezi kama akiba yake ya uzeeni, ni Sh2,000.

Hizi si pesa kidogo kwa Wakenya wengi ambao sasa hivi wanapambana na hali ngumu ya maisha. Japokuwa Sh2,000 hazinunui chakula cha siku moja kwa familia nyingi nchini, ni pesa ambazo zinahitajika kujalizia kwenye mahitaji ya msingi kama bei ya juu ya maji, stima, chakula na kadhalika.

Kisichofahamika na wengi ni kuwa, kwa kila pesa anazolipa mfanyikazi, mwajiri hutakiwa kuongeza kiwango sawa na hicho. Kwa sasa malipo ya lazima ni yake ya NSSF, Hazina ya Bima ya Taifa ya Afya (NHIF) na Mpango wa Malipo ya Kustaafu (RBA). Pesa hizo zote huwa mzigo kwa mfanyikazi na mwajiri wake. Kila mmoja hutoa kiwango sawa.

Wakati huu ambapo waajiri wanajikakamua kutofuta wafanyikazi baada ya athari za ugonjwa wa Covid-19, kuwaitisha malipo ya juu, huenda kukachangia baadhi yao kufunga biashara. Waajiri wengine watakaohisi kulemewa na malipo hayo, huenda wakafuta watu.

Hata kama watu watalipa ada hiyo mpya, kuna hakikisho gani kuwa pesa zao zitalindwa?

NSSF imekuwa ikikumbwa na kashfa moja baada ya nyingine. Ya punde zaidi ni kupatikana na hatia mameneja wake wanne kuhusiana na wizi kwenye ununuzi wa hisa za Sh1.4 bilioni.

  • Tags

You can share this post!

Nassir aendelea kubanwa kuhusu mawaziri wake

Vuguvugu jipya tishio kwa Azimio

T L