• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 5:06 PM
TAHARIRI: Mabishano kuhusu ushuru ni kejeli kwa raia wa Kenya

TAHARIRI: Mabishano kuhusu ushuru ni kejeli kwa raia wa Kenya

NA MHARIRI

KATIKA taifa lolote linalokusudia kujikuza kiuchumi, ukusanyaji ushuru huwa ni suala zito ambalo linalindwa kwa sheria kali.

Nchi zilizo mbele zaidi kimaendeleo kama vile Amerika na Uingereza huwa hazifanyi utani kuhusu masuala ya ushuru.

Wanaofuatilia habari za kimataifa wamewahi kushuhudia jinsi mabwanyenye na wanasiasa wengine mashuhuri katika mataifa aina hiyo huandamwa bila huruma kila inapobainika kwamba walikwepa kulipa ushuru.

Si walipaji ushuru pekee ambao huandamwa ili kuhakikisha wanatimiza sheria za kodi katika nchi hizo, bali pia raia wanaotakikana kuwasilisha ripoti zao za ushuru wakati wowote inapohitajika.

Tukirudi hapa nchini kwetu, hali ni ya kusikitisha. Kwa wiki chache zilizopita, suala la ushuru limegeuzwa kuwa la kisiasa ambapo wanasiasa wanalitumia kushambuliana kisiasa.

Matukio haya yamezua ubishi pia kuhusu matukio sawa na hayo ambayo yalikuwa yakishuhudiwa katika utawala uliopita, wakati ilipokuwa ikidaiwa kwamba wapinzani wa serikali hiyo walikuwa wanaadhibiwa kwa madai ya kukwepa kulipa ushuru.

Haya yote yanapotendeka, mwananchi wa kawaida hana namna ila kujiamulia kwamba kuna uwezekano mkubwa serikali zilizo mamlakani hujitolea kulinda watu fulani wenye mapato makubwa, iwe ni ya kibiashara au taaluma yoyote ile kukwepa kulipa ushuru.

Raia wa kawaida atasamehewa kuwa na dhana hii kwani matukio yanayoonekana kufikia sasa hayamruhusu kufikiria kivingine. Anajionea haya yote wakati ambapo yeye mwenyewe, kwa kiasi chake kidogo cha mapato, analazimika kukatwa ushuru wa asilimia kubwa ambao haumruhusu kubaki na fedha za kutosha kukimu mahitaji yake.

Anapotaka kugharimia mahitaji yake na familia yake nyumbani, bado anaandamwa na asilimia kubwa za ushuru wa bidhaa unaofanya bidhaa hizo kuwa ghali mno.

Zaidi ya hayo, anapopitiapitia taarifa za habari kwenye chombo chochote kile cha habari, hakosi kuona habari kuu inahusu mipango ya serikali kuongeza ada za bidhaa na huduma kama vile usambazaji wa umeme na maji.

Viongozi wa pande zote za kisiasa wanafaa kutambua hitaji la kuchukulia suala la ulipaji ushuru kwa uzito na wakome kulitumia kama silaha ya kushambuliana kisiasa.

Raia wengi wa kawaida walio mashinani hujitahidi sana kuhakikisha rekodi zao za ushuru hazina hitilafu, hasa wanapotambua kwamba hilo ni hitaji la kupata ajira serikalini kwa njia ya haki.

Viongozi wetu wawe mfano bora kwa kuadhibu kisheria yeyote kati yao anayekwepa kulipa ushuru, na kuhakikisha kuna haki katika viwango vyote vya ushuru vinavyotozwa humu nchini.

  • Tags

You can share this post!

Tottenham Hotspur wazamisha chombo cha Man-City katika EPL

CHARLES WASONGA: Serikali ya Ruto itahadhari isirudie...

T L