• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Tottenham Hotspur wazamisha chombo cha Man-City katika EPL

Tottenham Hotspur wazamisha chombo cha Man-City katika EPL

Na MASHIRIKA

BAO la Harry Kane ambaye sasa ni mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Tottenham Hotspur lilisaidia waajiri wake kukomoa Manchester City 1-0 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumapili.

Fowadi na nahodha huyo alicheka na nyavu za wageni wao katika dakika ya 15 baada ya kumegewa krosi safi na Pierre-Emile Hojbjerg. Hata hivyo, Spurs walikamilisha mechi na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya Cristiano Romero kuonyeshwa kadi ya pili ya manjano katika dakika ya 87.

Kane, 29, alitandaza mchuano wake wa kwanza kambini mwa Spurs mnamo Disemba 15, 2011. Bao lake dhidi ya Man-City ambao ni mabingwa watetezi wa EPL lilisisimua mashabiki walionyanyua na kibao kilichosoma “Hongera Harry Kane”.

Bao hilo la Kane lilikuwa lake la 200 katika EPL na sasa ndiye wa tatu katika orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa kipute hicho inayoongozwa na Alan Shearer (260) na Wayne Rooney (208).

Matokeo hayo ya Spurs yaliwadumisha katika nafasi ya tano kwa alama 39, moja pekee nyuma ya Newcastle United wanaofunga mduara wa nne-bora.

Kushindwa kwa Man-City kulinyima masogora hao wa kocha Pep Guardiola kupunguza pengo la alama kati yao na Arsenal ambao sasa wanaselelea kileleni mwa alama 50 licha ya Everton kuwapiga breki kali kwa kichapo cha 1-0 mnamo Jumamosi ugani Goodison Park. Man-City wanashikilia nafasi ya pili jedwalini kwa pointi 45.

Riyad Mahrez nusura asawazishie Man-City mwishoni mwa kipindi cha kwanza ila kombora lake likagonga sehemu ya chini ya mwamba wa goli la Spurs na mpira ukarejea uwanjani. Man-City hawajwahi kufunga bao wala kuondoka ugani Tottenham Hotspur na pointi yoyote kutokana na mechi tano zilizopita.

Kane alisherehekea bao lake sawa na ambavyo tineja wa umri wa miaka 18 angefanya – huo ndio umri aliokuwa nao alipofungia Spurs bao lake la kwanza miaka 12 iliyopita dhidi ya Shamrock Rovers katika Europa League.

Mabao 267 yanayojivuniwa na Kane ndani ya jezi za Spurs yametokana na mechi 416. Greaves alihitaji mechi 379 pekee kufungia kikosi hicho magoli 266.

Mechi kati ya Spurs na Man-City ilisimamiwa na kocha msaidizi Cristian Stellini aliyechukua mahali pa mkufunzi Antonio Conte aliyefanyiwa upasuaji wa kibofu nyongo hivi majuzi nchini Italia.

Mechi hiyo iliwapa Spurs fursa ya kulipiza kisasi dhidi ya Man-City waliotoka nyuma kwa mabao 2-0 na kuwatandika 4-2 katika mkondo wa kwanza wa EPL mnamo Januari 19, 2023 ugani Etihad.

Man-City watapania kujinyanyua upesi dhidi ya Aston Villa mnamo Februari 12 ugani Etihad kabla ya kuendea Arsenal uwanjani Emirates siku tatu baadaye.

Nottingham Forest walikomoa Leeds United 1-0 katika mechi nyingine ya EPL mnamo Jumapili ugani City Ground na kupaa hadi nafasi ya 13 jedwalini kwa alama 24 sawa na Crystal Palace. Leeds walisalia katika nafasi ya 17 kwa pointi 18 sawa na Everton.

MATOKEO YA EPL (Jumapili):

Nottm Forest 1-0 Leeds United

Tottenham 1-0 Man-City

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Watu 2,600 waaga dunia baada ya tetemeko kutokea nchini...

TAHARIRI: Mabishano kuhusu ushuru ni kejeli kwa raia wa...

T L