• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
CHARLES WASONGA: Serikali ya Ruto itahadhari isirudie makosa ya Jubilee

CHARLES WASONGA: Serikali ya Ruto itahadhari isirudie makosa ya Jubilee

NA CHARLES WASONGA

SERIKALI ya Kenya Kwanza inafaa kuacha taasisi huru za serikali zifanye kazi bila kuingiliwa wala kuelekezwa jinsi ambavyo viongozi wake wakuu wanavyofanya sasa.

Rais William Ruto, na wanasiasa wandani wake, wakome kabisa kuingilia majukumu ya asasi za serikali kwa kuzielekeza kuwaandama watu fulani wanaotofautiana nao kisiasa.

Wakiendelea kufanya hivyo, itaonekana kama wamegeuza asasi hizo kuwa silaha za kuwasaidia kuendesha vita vya kisiasa dhidi ya watu wanaowasawiri kuwa mahasidi wao kisiasa.

Ninakumbuka kuwa ni mtindo kama huu wa kutumia asasi za serikali kuendeleza vita vya kisasa ndio Dkt Ruto na wandani wake walidai Rais Kenyatta alitumia kunyanyasa washirika wake “bila sababu zozote maalum”.

Kwa mfano, Rais Ruto, na wandani wake, wanafaa wakome kuelekeza Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) jinsi ya kufanya kazi yake ya ukusanyaji kodi.

Ninadhani asasi hii inayo rekodi za kampuni zote nchini ambazo kwa sababu moja ama nyingine, hazilipi aina fulani za ushuru. Si kazi ya Rais Ruto na wanasiasa katika kambi yake, kukumbusha KRA kwamba kampuni hii au ile imekwepa ushuru hivyo basi kupaswa kushurutishwa ilipe.

Mamlaka ya KRA ina maafisa wake kote nchini ambao hutekeleza wajibu wa kukusanya ushuru kutoka kwa kampuni na biashara zote nchini. Majuzi akihutubia wabunge mjini Mombasa, Rais Ruto alimlenga mwanasiasa fulani ambaye alidai amekuwa akifadhili mikutano ya Azimio “ili aweze kukwepa kulipa ushuru”.

Lakini dakika chache baada ya Dkt Ruto kutoa kauli hiyo, maseneta John Methu (Nyandarua), James Murango (Kirinyaga) na Wahome Wamatinga (Nyeri) walihutubia kikao cha wanahabari katika jumba la KICC, Nairobi wakimshtumu Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, na familia yake, kwa kukwepa kulipa ushuru.

Watatu hao walidai, bila kutoa ithibati, kuwa Bw Kenyatta ndiye amekuwa akifadhili mikutano ya Azimio kama kinga ya kutolipa ushuru. Kauli za wanasiasa hao zilimfanya Mama wa Taifa wa zamani Mama Ngina Kenyatta kujitokeza waziwazi na kuishauri serikali kufuata mkondo wa sheria katika kuwaandama watu wanaodhani wa kuwa hawalipi ushuru.

Akiongea katika ibada eneo la Lamu, Mama Ngina alisema wale wasiolipa ushuru kwa njia moja ama nyingine washtakiwe kortini.

Na endapo watu kama hao watapatikana na hatia, Mama Ngina anashauri mali yao itwaliwe na kuuzwa ili kufidia ushuru ambao wangelipa.

Ninakubaliana na Mama Ngina kuwa suala la ushuru halifai kuwasilishwa katika majukwaa ya kisiasa na kutumiwa kuchafua majina ya watu machoni pa umma. Rais Ruto aelekeze juhudi zake katika mchakato wa kufanikisha utekelezaji wa ahadi walizowapa wananchi badala ya kujifanya kuwa ndio wanaelewa zaidi kazi ya asasi za umma kama KRA.

Pili, serikali ikome kutumia Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) kuwaandama wanasiasa wa Azimio kinyume cha sheria.

Hapa ninarejelea kisa cha juzi ambapo Diwani wa Wadi ya Korogocho, Bw Absalom Odhiambo alikamatwa nje ya afisi za Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC). Mwanasiasa huyo alikuwa amejiwasilisha kwa tume hiyo kuandikisha taarifa baada ya kuagizwa kufanya hivyo kufuatia matamshi aliyotoa katika mkutano wa Azimio yaliyofasiriwa kama ya kuchochea chuki.

Lakini baada ya diwani huyo kufikishwa katika mahakama ya Milimani, Nairobi, hakimu alimwachilia huru akidai kiongozi huyo alikamatwa kwa misingi ya sheria ambayo haipo.

Mifano miwili niliyotoa hapa inaonyesha wazi wazi kuwa serikali ya Kenya Kwanza imeanza kutenda maovu iliyoishutumu serikali ya Jubilee kutenda.

Ikiendelea kufanya hivyo, huenda serikali hii ikapoteza imani ya Wakenya haraka hata kuliko ile ya Jubilee.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Mabishano kuhusu ushuru ni kejeli kwa raia wa...

BENSON MATHEKA: Majangili kaskazini mwa Bonde la Ufa ni...

T L