• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
TAHARIRI: Magavana wapya waelimishwe kuhusu Sheria ya Ajira

TAHARIRI: Magavana wapya waelimishwe kuhusu Sheria ya Ajira

NA MHARIRI

WIKI jana na wiki hii serikali za kaunti zinaendelea kutangaza nyadhifa za watu watakaokuwa mawaziri au makatibu wa Kaunti.

Nyadhifa hizo zinajazwa kwa mujibu wa katiba kwamba serikali ya kaunti inapounda upya, gavana mpya anaruhusiwa kuunda Baraza la Mawaziri analotaka.

Kwenye matangazo ambayo yamekuwa yakichapishwa magazetini, inaonekana wasimamizi wa kaunti hawajaelewa kwamba sheria inayohusu ajira ilifanyiwa marekebisho mwaka huu.

Matangazo hayo yanaeleza kuwa ni lazima anayetaka nafasi hiyo ajumuishe vyeti vya kuonyesha anatimiza matakwa ya Sura ya Sita ya Katiba kuhusu maadili.

Hali halisi ilivyo ni kuwa, mnamo mwezi Aprili mwaka huu, Rais Uhuru Kenyatta alitia saini marekebisho ya sheria za uajiri na kufanya isiwe lazima kwa anayeomba kazi serikalini kuwasilisha vyeti hiyo, isipokuwa iwapo ameorodheshwa kwa mahojiano.

Sheria hiyo inayojulikana kama The Employment (Amendment) Act, No. 15 of 2022 ilipendekezwa na aliyekuwa Mbunge Maalum Bw Gideon Keter.

Alipokuwa akiwasilisha mapendekezo hayo Bungeni, Bw Keter alisimulia jinsi yeye binafsi na maelfu ya vijana walivyokuwa wakiporwa pesa kwa kulipia vyeti ambapo baadaye hawapewi ajira.

“Mtu angetumia hadi Sh6,000 akilipia vyeti pekee. Hata kama cheti ha Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) hupeanwa bila malipo, bado kuna pesa za kumlipa wakili ili akugongee muhuri. Iwapo unaishi vijijini, kumpata wakili ni sharti usafiri hadi mjini. Hapo, panahitajika nauli. Unatumia pesa hizi zote ilhali hakuna hakikisho kuwa utapewa hiyo kazi,” aliwahi kusema Bw Keter alipokuwa akiunga mkono marekebisho hayo.

Vyeti vinavyohitajika ni kile cha EACC, cha kuonyesha mtu analipa ushuru kwa KRA, cha kuonyesha ni mlipaji madeni (CRB), kwamba hana rekodi za uhalifu (DCI) na kwamba mtu amekuwa akilipa mkopo wa masomo ya Chuo Kikuu (HELB).

Ingawa sheria hiyo inalenga kuwalinda vijana wanaotafuta kazi dhidi ya kupunjwa, inafaa kutekelezwa kwa watu wote wanaotafuta kazi za umma.

Maafisa wa masuala ya sheria katika kaunti wanapaswa kusoma kwa makini sheria na kuwashauri magavana na wakuu wengine wa kaunti wanapoandika matangazo ya ajira.

Wanapaswa kufahamu kwamba sheria hii inawalazimu watu walioorodheshwa kwa mahojiano pekee, kuwa wanaolazimika kuwasilisha vyeti, na si kila muombaji.

Magavana wapya hawana budi kuanza kujifunza sheria. Majukumu yao mengi yanaongozwa na sheria, na katu hakutakuwa na njia ya mkato, isipokuwa kutekeleza sheria kikamilifu.

You can share this post!

Uamuzi unaotarajiwa kutolewa kesho utahusisha masuala tisa

MIKIMBIO YA SIASA: Kamket aliichakaza Kanu bondeni kwa...

T L