• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 7:50 AM
TAHARIRI: Mazimwi yanayokula soka yetu yazimwe

TAHARIRI: Mazimwi yanayokula soka yetu yazimwe

Na MHARIRI

KATIKA hatua ya kutanzua kilichodororesha viwango vya kandanda nchini, itakuwa bora kutazama kitu ambacho mataifa mengine yanafanya ambayo hatufanyi sisi.

Kauli hii inachochewa na mwanguko mkubwa wa hadhi ya soka ya Kenya kwa sasa unapolinganisha na miaka ya ’70 na ’80 ambapo mataifa mengi barani Afrika yaliziogopa sana timu za Kenya; iwe ni timu ya taifa Harambee Stars au klabu hasa AFC Leopards na Gor Mahia.

Aidha, matokeo ya timu zetu zinazotuwakilisha katika mitanange ya kimataifa hayaridhishi hata kamwe wala timu za mataifa mengine haziogopi tena zinazopokabidhiwa timu yoyote ya Kenya.

Kwa sasa Gor Mahia na Tusker zinawakilisha taifa hili katika mashindano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baina ya kalbu.

Hata hivyo, unapoyatazama matokeo ya duru ya kwanza, Gor Mahia walibamizwa japo kwa bao 1-0 na klabu ya AS Otoyo ya Congo (Brazzaville) huku Tusker wakilazimishwa kula sare tasa na SC Sfaxien ya Tunisia.

Sifa mbovu ya Harambee Stars inajulikana; majuzi zaidi imebanduliwa kiaibu katika michuano ya kufuzu kwa Kombe la Dunia, miezi michache baada ya kukosa tiketi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika mapema mwaka ujao 2022.

Kwa tathmini ya mbali, klabu mbili; Gor Mahia na Tusker, zina nafasi finyu sana ya kupiga hatua katika kandanda hiyo ya CAF hasa inapochukuliwa kuwa Wanamvinyo wanacheza ugenini baada ya kuambulia sare nyumbani huku Gor ambayo japo ina nafasi bora kidogo kwa sababu inachezea nyumbani, lolote laweza kufanyika hadi Otoyo ikapiga hatua nayo Gor ibanduka.

Hali hii inaturejesha katika swali; udhaifu wetu uko wapi hasa?

Wataalamu wametaja mfumo wa kukuza vijana chipukizi hadi katika viwango vya kitaifa kama tatizo kuu linalotesa nchi hii.

Wanaeleza kuwa hatuna urasmi wowote unaoweza kusaidia kuibua talanta thabiti kutoka mashinani kinyume na mataifa mengine ambayo soka yao imepiga hatua ya maana kama vile Uingereza na barani Ulaya kwa jumla.

Miungomsingi duni ni tatizo la pili. Serikali ya Jubilee ilinoa pakuwa katika hili. Taifa hili halina viwanja vya kutosha vya kuwezesha mafunzo ya kitaalamu kwa wanamichezo wetu.

Japo serikali kadhaa za kaunti zimefanya kazi nzuri, jitihada za magatuzi pekee hazitoshi; zahitaji mchango wa serikali ya kitaifa.

Tatizo la ufisadi na uongozi duni hasa miongoni mwa viongozi wa shirikisho la soka FKF linafaa kuzimwa iwapo taifa hili lina matumaini yoyote ya kufika mbali katika si mchezo wa kandanda pekee bali katika tasnia nzima ya spoti.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Ili kufikia hadhi iliyotwikwa, Nakuru iyaige...

Mwanaharakati mashuhuri David Kimengere arejea nchini baada...

T L