• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
TAHARIRI: Mbinu kukabili upangaji mechi FKF ziwe pana

TAHARIRI: Mbinu kukabili upangaji mechi FKF ziwe pana

NA MHARIRI

WIKI jana, Shirikisho la Soka Nchini (FKF) liliwapiga marufuku makocha na wachezaji, 15 ambao lilidai walihusishwa na upangaji wa matokeo ya mechi katika ligi mbalimbali za Kenya.

Kwenye orodha hiyo walikuwepo beki wa Tusker Isaac Kipyegon na kiungo wa zamani wa Nairobi City Stars Mike Madoya ambaye alikuwa Mchezaji Bora wa Msimu (MVP) msimu wa 2016/17 na aliyekuwa kocha wa makipa Gor Mahia Willis Ochieng’ miongoni mwa wengine.

FKF iliwazuia 15 hao kujihusisha na soka hadi uchunguzi kuwahusu ukamilike na hatima yao kufahamika.

Hata hivyo, Madoya na Kipyegon walielekea Jopo la Kutatua Mizozo ya Michezo Nchini (SDT) na wamepata amri ya kuzuia FKF kuwachunguza hadi kesi yao isikizwe na iamuliwe.

Donda sugu hili la upangaji wa matokeo ya mechi linastahili kuvaliwa njuga ila badala ya wachezaji kutwikwa lawama zote, FKF yenyewe haifai kusazwa na inastahili kulaumiwa pia.

Upangaji wa matokeo nchini huhusisha wachezaji, makocha, wachezaji wa zamani, wanahabari, marefa, wanahabari na hata baadhi ya maafisa wa shirikisho.

Kwa hivyo, hili ni tatizo ambalo limezama ndani ya fani ya soka ambalo linahitaji kutafutiwa suluhu ya kudumu.Kuhusu FKF, ni aibu kuwa inawahukumu wanaodaiwa kuhusika ilhali shirikisho lenyewe halijawalipa marefarii mshahara wao kwa muda wa miezi mitano iliyopita.

Marefa wenye njaa hawawezi kukataa kuhongwa ili kupendelea timu fulani kwa kuwa hata wao wana familia ambazo zinawategemea na lazima wasake hela za kuwakimu vizuri.

Kumekuwa na madai ya maamuzi ya kibaguzi hata katika mechi ya katikati ya wiki hii ya KPL, baadhi ya timu zikilalamikia kuonewa kwa marefa.

Tabia hii bado itaendelea kujitokeza iwapo FKF haitawalipa marefa mishahara yao.

Vivyo hivyo, wachezaji na makocha hawawezi kuzingatia nidhamu iwapo hawalipwi mishahara na klabu zao. Timu kama FC Talanta ambayo inashiriki KPL imeathiriwa vibaya kwa kuwa haijawalipa wachezaji mishahara kwa miezi minane iliyopita.

Kama tu refa, mchezaji au kocha ambaye ana njaa lazima atakiuka maadili ya taaluma hii na kushiriki upangaji wa matokeo ya mechi kupata fedha. Wanahabari nao hawajaachwa nyuma kwa kuwa imebainika baadhi yao wenye tamaa hujihusisha na kamari kisha hugawa pesa na wachezaji baada ya ubashiri wao kutimia.

Kunastahili kuwe na adhabu kali kwa wanaopatikana wanashiriki upangaji wa matokeo ya mechi ikiwemo kupigwa marufuku ya kutojihusisha na soka maishani.

Hata hivyo, uchunguzi kuhusu suala hili unastahili kuwa wandani kupata wahusika badala ya kuwahukumu tu wale ambao huenda wasiwe na hatia.

Pia FKF iwe ikitoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wachezaji, makocha, marefa na washikadau wote wa soka kuhusu athari ambayo upangaji wa matokeo ya mechi unaweza kuwa nao katika taaluma zao.

  • Tags

You can share this post!

EPL: Wikendi ya kufa kupona

Wavulana wengi wakosa kufanya KCSE baada ya kusajiliwa

T L