• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:50 AM
EPL: Wikendi ya kufa kupona

EPL: Wikendi ya kufa kupona

BAADA ya mabingwa watetezi Manchester City kulipua Tottenham Hotspur 4-2 Alhamisi, leo ni zamu ya miamba Liverpool na Chelsea.

Makocha Graham Potter, Jurgen Klopp, Frank Lampard, David Moyes na Brendan Rodgers wako hatarini kupoteza kazi zao kutokana na msururu wa matokeo ya kusitikisha. Liverpool wako nambari 9 nao Chelsea 10.

Miamba Liverpool na Chelsea watafungua ratiba ya leo saa tisa unusu. Watajibwaga uwanjani Anfield wote wakiwa na alama 28.

Kila mmoja anaendea koo la mwenzake akitumai kujinasua na kutumbukiza mwenzake pabaya zaidi. Vijana wa Potter walipasha misuli moto kwa kunyuka Crystal Palace 1-0.

Liverpool walinyolewa bila maji 3-0 na Brighton, wikendi iliyopita. Chelsea inatarajiwa kuanzisha sajili mpya Mykhailo Mudryk.

Vijana wa Klopp walilima Wolves 1-0 kwenye Kombe la FA Jumanne. Macho yatakuwa kwa mvamizi Mohamed Salah. Reds walipanguliwa 1-0 na Blues mara ya kwisho walikutana ligini.

Wakati huo huo Bournemouth nambari 17 itakutana na Nottingham Forest nambari 13. Cherries ni wenyeji wa Nottingham uwanjani Vitality. Wako pabaya.

Vijana wa kocha Gary O’Neil wamepoteza michuano sita mfululizo katika mashindano yote. Wana alama 16. Bournemouth walilemewa 2-0 na Brentford Jumamosi iliyopita.

Nottingham wameamka baada ya kuanza msimu vibaya. Walibandua Wolves kipute cha Carabao na kuduwaza Leicester 2-0 ligini. Wana pointi 20.

Bournemouth wamekanyaga Nottingham mara mbili mfululizo. Washambulizi Philip Billing (Bournemouth) na Brennan Johnson (Nottingham) watategemewa. Nayo Leicester inaalika Brighton ugani King Power. Foxes hawajaokota alama mara nne mfululizo ligini.

Mashabiki wenye hasira waliitisha Rodgers afutwe kazi baada ya kupoteza mikononi mwa Nottingham. Brighton wamekuwa katili zaidi chini ya kocha Roberto De Zerbi. Walikung’uta Liverpool 3-0, wikendi iliyopita.

Brighton wanafukuzia ushindi wa nne katika mashindano yote.Matumaini ya Seagulls kuingia mashindano ya Ulaya yako hai. Watapiga hatua kubwa wakizima Foxes iliyopoteza 5-2 katika mkondo wa kwanza.

Mechi nyingine ni kati ya Southampton (20) v Aston Villa (11): Wavuta-mkia Southampton wako mawindoni kulipiza kisasi.

Walipoteza mechi mbili zilizopita dhidi ya Villa kwa jumla ya magoli 5-0. Saints walikaribisha kocha mpya Nathan Jones kwa kupepeta Everton 2-1.

Wanatafuta ushindi wa nne mfululizo baada pia kunyamazisha Crystal Palace (Kombe la FA) na Manchester City (Carabao). Villa ya kocha Unai Emery ilizamisha Leeds 2-1 katika mechi iliyopita. James Ward-Prowse amekuwa akifanyia Saints makubwa.

Villa inajivunia kuwa na winga matata Leon Bailey. West Ham (18) v Everton (19): Makocha David Moyes (West Ham) na Frank Lampard (Everton) wako roho mkononi.

Kwa sasa wako hatarini kuachishwa kazi kwa sababu ya matokeo duni.Tetesi zinasema West Ham inamezea mate Nuno Espirito Santo, Rafael Benitez au Sean Dyche kuingia nafasi ya Moyes. Winga Said Benrahma anasema yuko tayari kupigania West Ham kuona inajiondoa pabaya.

Leeds, Leicester, Wolves, Bournemouth, West Ham, Everton na Southampton wako katika vita vikali vya kutemwa.

Dejan Kulusevski na Emerson Royal walipatia Spurs uongozi wa 2-0 wakati wa mapumziko kabla ya City kujibu katika kipindi cha pili kupitia kwa Julian Alvarez, Erling Haaland anayeongoza ufungaji wa mabao (22), na Riyad Mahrez aliyetetemesha nyavu mara mbili.

Licha ya ushindi huo unaokata uongozi wa Arsenal kutoka pointi nane hadi tano, kocha Pep Guardiola alieleza kusikitishwa na vijana wake kutoonyesha ari ya kupigana.

  • Tags

You can share this post!

West Ham United wajinasia huduma za Danny Ings kutoka Aston...

TAHARIRI: Mbinu kukabili upangaji mechi FKF ziwe pana

T L