• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 2:31 PM
TAHARIRI: Nchi itanawiri zaidi tukiwapa wanawake nafasi

TAHARIRI: Nchi itanawiri zaidi tukiwapa wanawake nafasi

NA MHARIRI

KATIKA miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na maendeleo makubwa sana kuwahi kupigwa na wanawake katika sekta mbalimbali za maisha.

Maendeleo haya yamechochewa na kuboreka kwa mazingira yanayowaruhusu wanawake kuwa huru zaidi ili kutoa mchango muhimu katika maendeleo ya jamii.

Katika ngazi ya kimataifa, taifa lenye nguvu duniani la Amerika lina makamu wa rais mwanamke, Khamala Harris. Uteuzi wake kuwa mgombea mwenza wa Rais Joe Biden ulikuwa miongoni mwa sababu kuu zilizowashawishi raia wengi wa taifa hilo kuwapigia kura.

Barani Afrika katika mataifa jirani, Rais wa Ethiopia ni mwanamke. Katika nchi ya Tanzania, rais wa sasa aliyetwaa nafasi baada ya kifo cha John Magufuli, Bi Samia Suluhu ni mwanamke.

Tukija nchini Kenya, ipo idadi nzuri tu ya wanawake wanaoshikilia nyadhifa za hadhi kuu. Katika uchaguzi wa 2017, tuliweka historia kwa kuwachagua wanawake watatu kuwa magavana.

Charity Ngilu wa Kitui, Joyce Laboso wa Bomet (sasa marehemu) na Anne Waiguru wa Kirinyaga daima watasalia katika mabuku ya kumbukumbu. Baada ya kung’atuliwa mamlakani gavana wa Nairobi Bw Mike Sonko, Bi Anne Kananu aliteuliwa kuongoza kaunti hii ya jiji.

Idara ya mahakama ambayo ni mhimili mmojawapo kati ya mitatu ya serikali inaongozwa na mwanamke. Bi Martha Koome ndiye Rais wa mahakama nchini. Katibu wa mahakama Bi Ann Amadi vilevile ni mwanamke.

Wengi wa wanawake hawa ambao wamejaaliwa kupata nafasi za kuhudumia jamii katika ngazi mbalimbali wamedhihirisha ukomavu wa hali ya juu na kufanya kazi kwa uadilifu.

Maadamu lipo hitaji la kisheria kwamba nafasi zote za uongozi ziwe na uteuzi au za kuchaguliwa hazifai kuwa na zaidi ya theluthi moja ya jinsia moja, wanawake wana kila sababu ya kushiriki kwa wingi katika uchaguzi mkuu ujao. Tunatarajia kwamba wanawake zaidi watachaguliwa kwa sababu pia ni wanawake ndio wengi nchini katika idadi.

Baada ya uchaguzi, tunatarajia pia kwamba chama kitakachounda serikali kitateua wanawake wengi katika nafasi za uongozi. Katika uzi huu huu, tunampongeza naibu rais Dkt William Ruto kwa kuahidi kwamba endapo atashinda uchaguzi mkuu ujao, atateua wanawake 10 katika baraza lake la mawaziri.

Hatua zaidi ilipigwa Jumatatu baada ya mgombea urais kwa tiketi ya Azimio la Umoja Bw Raila Odinga kumteua Bi Martha Karua kuwa mgombea mwenza wake.

Kadri wanawake zaidi wanaposhirikishwa katika masuala ya uongozi, ndivyo nchi itapiga hatua kubwa zaidi za maendeleo.

  • Tags

You can share this post!

Karua alazimisha Ruto kufanya hesabu upya

CECIL ODONGO: Jamii ya Mulembe isake msemaji mwengine baada...

T L