• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 7:22 PM
TAHARIRI: Ni fedheha wanasiasa kufadhili wahuni

TAHARIRI: Ni fedheha wanasiasa kufadhili wahuni

NA MHARIRI

TUKIO la mnamo Jumatatu ambapo wahuni, walioonekana kufadhiliwa na mahasimu wa kisiasa wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na kinara wa Azimio la Umoja Raila Odinga, litaipaka tope nchi hii katika midani ya kimataifa.

Wahuni hao walivamia shamba la familia ya Kenyatta eneo la Kamakis, Eastern By-pass, Kaunti ya Kiambu, na kukata miti, kuchoma shamba hilo la miti na kuiba mamia ya kondoo.

Magenge hao wakiendelea na uovu huo bila kuzuiwa na maafisa wa usalama, wengine jijini Nairobi walijaribu kuvamia kampuni ya Bw Raila ya Spectre Limited japo walishindwa kuingia ndani na hivyo kuamua kutupia jengo hilo mawe ambayo yalivunja vioo vya madirisha.

Uvamizi huo uliripotiwa kwingi na vyombo vya habari, si Kenya tu bali kwingineko duniani. Vyombo maarufu vya habari vya kimataifa kama vile BBC na CNN vilipeperusha habari hizo vikisema magenge hayo ya wahuni yalifadhiliwa na serikali.

Kwa kuripoti hivyo, sifa ya Kenya katika mataifa ya kigeni iliharibiwa vibaya sana kiasi kwamba waziri wa Masuala ya Kigeni nchini Ujerumani aliamua kufutilia mbali kikao cha pamoja na Rais William Ruto kilichokuwa kimeratibiwa jana. Kikao hicho bila shaka kilifutiliwa mbali kutokana na matukio hayo ya magenge. Japo Ujerumani ndiyo iliyokuwa imechukua hatua kufikia jana tukienda mtamboni, mataifa mengine pia, hasa yenye ushawishi mkubwa ulimwenguni, yalitarajiwa kuwekea Kenya vikwazo au viongozi wake hasa wa serikali.

Ni fedheha kuwa matukio hayo ya uhalifu yalifanyika huku maafisa wa usalama wakitazama bila kuchukua hatua. Iliripotiwa kuwa maafisa wa usalama walifika penye uvamizi jana, takribani saa 24 baada ya tukio hilo kufanyika.

Huu ni mkondo usiopendeza hata kidogo kwani unaweza kuchangia kuzuka kwa vita baina ya matabaka; wenye uwezo kiuchumi na hohehahe.

Mbali na uhalifu huo, pia ripoti zilieleza kuwa magenge yalifadhiliwa ili kuwaibia na kuwajeruhi wanahabari waliokuwa wakiangazia maandamano ya Azimio hasa katika mitaa ya Kibera na Mathare. Iliripotiwa kuwa maafisa waliokuwa wameshika doria katika eneo la Kibera walikuwa wakiwaruhusu wanahabari kuingia ndani ya mtaa ambao watu walikuwa wamejifungia ndani, huku wakijua huko ndani kulikuwa na magenge yaliyoonekana kufadhiliwa kuwapiga wanahabari na kuwaibia mali yao.

Huu ni mkondo hatari ambao ukiruhusiwa kutamalaki, basi tutarajie maharibifu makubwa na hata ghasia nchini hivi karibuni.

  • Tags

You can share this post!

‘Kaunti jirani zipige jeki Coast General’

TANZIA: Mbunge afariki baada ya kugongwa na pikipiki

T L