• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
TAHARIRI: Rais ‘sema’ neno moja tu raia wasife njaa tukiona

TAHARIRI: Rais ‘sema’ neno moja tu raia wasife njaa tukiona

NA MHARIRI

YEYOTE aliyeyasoma makala maalum yaliyochapishwa katika gazeti la Daily Nation toleo la Jumatatu, haikosi alitekwa na taswira ya kuhuzunisha na kusikitisha iliyoibuliwa na picha ya mtoto aliyejiinamia kwa magoti, dhahiri shahiri akikeketwa na njaa; yu hoi si wa jana si wa leo.

Mtoto huyo aliyedhoofishwa sana na njaa ni dhihirisho mwafaka la hali ilivyo katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

Wala njaa hiyo haiko Kenya tu, imeathiri mataifa mengi ya ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara kama vile Ethiopia, Sudan, Somalia na hata Uganda.

Ukosefu wa chakula na maji katika maeneo ya Kaskazini Mashariki umetokana na kiangazi cha takribani miaka minne; hali iliyochangia kuangamia kwa mifugo wengi pamoja na wakazi.

Wala si siri kuwa Wakenya wanakufa kwa njaa, ni bayana kuwa watu wengi wameenda jongomeo kutokana na makali ya janga hilo. Naam, mtu mwenye njaa ywaweza kufa kwa urahisi akipatwa na ugonjwa kuliko mwenye shibe.

Unapoanza kuyasoma makala hayo, unajiuliza kwa nini hakuna jitihada zinazoanzishwa kuchangia waathiriwa wa ukame na njaa pesa zinazoweza kuokoa wengi wao ambao vinginevyo watatangulia mbele ya haki?

Tunasadiki kuwa wapo Wakenya wengi wenye roho karimu wanaoweza kujitolea kuchanga pesa za kuwaokoa wenzetu katika maeneo ya Kaskazini Mashariki. Hatua hii imewahi kuchukuliwa hapo awali na kwa hakika tunaamini ilisaidia wengi kukwepa mauti.

Hii haina maana kuwa serikali ikae raha mstarehe bila kutekeleza jukumu la kuwalinda Wakenya. Sharti itie juhudi zaidi kuhakikisha kila mwathiriwa anapata msaada unaotolewa.

Shehena ya mwisho kutumwa na serikali ya Rais William Ruto katika maeneo yaliyoathiriwa ilisafirishwa hadi maeneo hayo zaidi ya majuma matatu yaliyopita.

Kwa hivyo kuna uwezekano mkubwa kuwa chakula na bidhaa nyingine za msaada zilizotolewa na serikali ama hazikuwafikia walengwa wote au waliosaidiwa walikila wakakimaliza, hivyo basi kuibua shinikizo za serikali kutuma shehena nyingine.

Pia yapo mashirika kadhaa yasiyokuwa ya kiserikali ambayo yamekuwa yakiwasaidia waathiriwa. Lakini wahisani hao peke yao hawawezi kushinda njaa inayowavuruga Wakenya wenzetu.

Sharti juhudi zifanywe kutoka pembe mbalimbali ili kuwaokoa wahasiriwa wasife ilhali baadhi ya Wakenya wana mabilioni au mamilioni ya pesa, mbali na kuwa na moyo wa hisani.

Rais Ruto anaweza kuanzisha mkakati wa kusaidia serikali yake kuwalisha walioathiriwa.

You can share this post!

Njaa yapunguza pakubwa idadi ya watoto katika shule za Pokot

CECIL ODONGO: Miguna hatoshi kumbandua Raila ubabe wa siasa...

T L