• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:24 PM
CECIL ODONGO: Miguna hatoshi kumbandua Raila ubabe wa siasa Nyanza

CECIL ODONGO: Miguna hatoshi kumbandua Raila ubabe wa siasa Nyanza

NA CECIL ODONGO

TANGU kurejea kwa mwanaharakati Miguna Miguna wiki jana, gumzo limetanda mitandao ya kijamii kwamba wakili huyo yupo pazuri kurithi ubabe wa Raila Odinga katika siasa za eneo la Luo Nyanza.

Miguna ameishi uhamishoni kwa karibu miaka minne tangu afurushwe na uliokuwa utawala wa Jubilee baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Mwanasiasa huyu kidomodomo amekuwa hasidi mkubwa wa Bw Odinga; licha ya kwamba kwa wakati fulani wawili hao walifanya kazi pamoja, katika Serikali ya Muungano ya Rais mstaafu marehemu Mwai Kibaki na Bw Odinga.

Mwanzo, kuna uwezekano ushawishi wa Bw Odinga ukapungua katika ngome zake kama Nyanza baada ya kushindwa urais kwa mara ya tano, ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Hata hivyo, hilo pia bado litategemea karate za kisiasa ambayo Waziri Mkuu huyo wa zamani atacheza kuelekea uchaguzi wa 2027.

Pili, kupiga kelele mitandaoni na kuibua utata au kugombana na kila mtu, hakutoshi kumpa Miguna udhibiti wa jamii ya Luo kisiasa.

Hata Bw Odinga mwenyewe hakuteuliwa na mtu yeyote kuwa kigogo wa siasa za Nyanza baada ya kifo cha marehemu babake Jaramogi Oginga Odinga mnamo Januari 1994.

Itakumbukwa kwamba wakati huo kulikuwa na wanasiasa wengine ndani ya Ford Kenya ambao walikuwa na ushawishi zaidi yake; kama Gavana wa Siaya James Orengo na mwenzake wa Kisumu Profesa Anyang’ Nyong’o.

Kati ya maamuzi magumu ambayo Bw Odinga alifanya ni kujiuzulu kutoka Ford Kenya na ubunge wa Langata, baada ya mzozo kuchacha kati yake na nyapara wa chama hicho mwendazake Wamalwa Kijana.

Baadaye alisaka kiti hicho kupitia chama cha NDP na kukishinda; huo ukawa mwanzo wa safari yake ya kutwaa udhibiti wa siasa za Nyanza.

Je, ni mwanasiasa gani kwa sasa anaweza kukubali kurudi kwa debe katika uchaguzi mdogo ili kupigania kiti alichokishinda, eti kwa sababu amekosana na uongozi wa chama kilichomdhamini?

Raila alipigania nafasi yake katika uongozi wa Waluo na Kenya nzima – kutokana na maamuzi ya kisiasa aliyoyafanya na uanaharakati wa kukomboa taifa kutoka kwa utawala dhalimu wa Kanu.

Pia, alihakikisha anachangia kudumisha utangamano huo wa taifa na kutoa uongozi unaohitajika kwa wakati ufaao, mara nyingine hata kujinyima.

Je, Miguna ameifanyia nini jamii ya Luo na taifa kwa jumla hata wakati alikuwa katika Serikali ya Muungano, kiasi cha kumfanya ajione mkombozi wa Waluo kutoka kile anachodai ni minyororo ya familia ya Odinga.

Iwapo Miguna anataka kuwa nyapara wa siasa za Waluo, basi atalazimika kukomesha siasa zake za matusi na kutetea maslahi ya jamii kiungwana.

Pia ufuasi haupatikani katika mitandao ya jamii bali arejee nyumbani na kushauriana na wakazi kisha aridhiane na Bw Odinga.

Kwa sasa kuna dhana Ujaluoni kuwa Miguna ni msaliti anayefurahia madhila ya jamii hiyo baada ya kukosa urais.

Hata hivyo, akikumbatia na kuridhiana na Bw Odinga atajitakasa wala hatakuwa wa kwanza kufanya hivyo.

Mabw Orengo, Nyong’o na hata Raphael Tuju walikuwa mahasimu wakubwa wa Bw Odinga lakini wakaridhiana naye na kile kilichoonekana kama usaliti wao kutokomea.

Kwa sasa na jinsi anavyoendelea kumdhalilisha Raila, Miguna na baadhi ya viongozi waasi wanaoegemea serikali wana nafasi finyu sana kurithi ufalme wa Bw Odinga katika siasa za Nyanza.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Rais ‘sema’ neno moja tu raia wasife njaa...

WANDERI KAMAU: Mauaji ya mwanahabari wa Pakistan nchini...

T L