• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 8:50 AM
TAHARIRI: Serikali ijayo izibue mifereji ya pesa kwa kaunti

TAHARIRI: Serikali ijayo izibue mifereji ya pesa kwa kaunti

NA MHARIRI

UTAWALA wa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto ndio huo unaelekea ukingoni na wachanganuzi na wanahistoria watakuwa na mengi ya kusema kuhusu waliyotekeleza na waliyoshindwa kabisa kufanikisha licha ya ahadi na matarajio mengi.

Lakini kati ya yote ambayo yatazungumziwa, lile la kufaulisha ugatuzi pengine litaacha wengi na manung’uniko mengi.

Ama kwa kweli, endapo kuna kitu serikali mpya ijayo itastahili kurekebisha upesi na kikamilifu, ni mfumo wa utoaji wa fedha za maendeleo kwa Kaunti.

Ripoti ya mashirikia mawili ya kiutafiti ambayo yamechanganua utendakazi wa mfumo wa mgao wa fedha kati ya Serikali Kuu na zile za Kaunti kati ya 2014 na 2020 inaonyesha kwamba mazoea ya ucheleweshaji wa pesa kwenda kwa kaunti na kupunguza mgao wenyewe umechangia kaunti nyingi kukosa kufadhili miradi ya maendeleo huku pesa zilizopatikana zikienda kulipa mishahara pekee.

Mashirika ya Masuala ya Uchumi (IEA) na Urban Institute yanasema kuwa matokeo yamekuwa kupungua kwa idadi ya kaunti zinazotumia kiwango kilichowekwa kisheria (asilimia 30 ya mapato) kufadhili maendeleo, kutoka 31 mnamo 2014, hadi kaunti 13 pekee kufikia 2020.

Wengi wanaofanya kazi katika kaunti wanalia kila kukicha kuhusu kucheleweshwa kwa mishahara yao. Wengine wengi wanalalamikia kupunga hewa ofisini bila kazi yoyote ya kufanya kwa sababu idara zao hazijapata pesa za kutekeleza miradi yoyote ya maendeleo.

Wengine hata huamua kuacha kazi na kutafuta kwingine wakilalamikia kukosa nafasi ya kuonyesha ujuzi wao wa kikazi.

Si ajabu kwamba kati ya masuala ambayo yalipigwa vita na kukejeliwa pakubwa wakati wa mchakato wa kubadilisha Katiba almaarufu BBI, lilikuwa lile la kuongeza mgao kwa kaunti. Wengi waliuliza mgao ungeongezwa kivipi ilhali huu uliopo wala haufikii kaunti katika muda unaopaswa?

Kisha maswali yanaibuka, kuhusu idadi ya wananchi ambao maisha yao yangeimarika endapo tu kaunti zao zingepokea mgao wao kwa muda unaofaa na kwa kiwango hitajika.

Unajiuliza ni ‘bodaboda’ wangapi wangepata vitengo vya kuegesha pikipiki zao wakisubiri wateja. Unajiuliza ni ‘mamamboga’ wangapi wangepata vibanda vya kisasa ambavyo wanaweza kuuza bidhaa zao kwa usalama na ustaarabu zaidi. Ni miundomsingi mingapi ingebadilika katika kila wadi na kaunti, kwa kupokea ufadhili inavyostahili.

Na ingawa suala la ufisadi bado ni dondandugu, litakabiliwa ipasavyo na asasi zilizopo kwa sababu taratibu zitakuwa zimenyooka na wakuu wa kaunti watakuwa katika nafasi ya kumulikwa kuwajibishwai zaidi bila vijisababu.

  • Tags

You can share this post!

Sonko kuwania ugavana Mombasa kupitia Wiper

TANZIA: Rais Mstaafu Mwai Kibaki amefariki dunia

T L