• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 4:43 PM
Sonko kuwania ugavana Mombasa kupitia Wiper

Sonko kuwania ugavana Mombasa kupitia Wiper

NA JUMA NAMLOLA

SIASA za Ugavana Mombasa zinatarajiwa kupamba moto, baada ya chama cha Wiper kumkabidhi aliyekuwa gavana wa Nairobi, Mike Mbuvi Sonko tikiti ya kupeperusha bendera ya chama hicho.

Mwanasiasa huyo aliyekihama chama cha Jubilee wiki chache zilizopita, jana alikabidhiwa cheti cha kuwania ugavana na kinara wa Wiper, Stephen Kalonzo Musyoka.

Kwenye hafla hiyo katika makao ya shughuli za kisiasa za Wiper, Nairobi, Mbunge wa Kisauni Bw Ali Mbogo alipewa cheti cha kuwa mgombea mwenza.

Hatua hiyo ya Alhamisi inamaliza mzozo uliokuwa umeibuka Mombasa kuhusu mwaniaji wa Wiper, baada ya chama hicho awali kumpa Bw Mbogo tikiti.

“Nilipewa cheti cha muda kama mgombea wa Wiper bila kupingwa kuwania kiti cha ugavana Mombasa. Tunachosikia kuhusu Sonko ni uvumi tu. Sina mpinzani katika chama cha Wiper na hakutakuwa na uteuzi Mombasa,” akasema Bw Mbogo wakati huo.

Lakini jana, Bw Musyoka alifafanua kuwa, cheti alichokuwa amepewa Bw Mbogo kilikuwa cha muda, na wakati huo hakukuwa kumejitokeza mtu mwingine katika chama hicho.

“Kwa kifupi, nawatangazia Wakenya na wakazi wa Mombasa kwamba, mheshimiwa Gavana Sonko na mheshimiwa Ali Mbogo wamekubaliana, kuwania kwa tikiti moja ya Wiper. Najua tayari Mombasa kuna msisimko,” akasema Bw Musyoka.

Alieleza kuwa, kwa kuwa Bw Sonko alihudumu muhula mmoja Nairobi, kisheria, iwapo atachaguliwa Mombasa atahudumu kwa miaka mitano pekee.

Alieleza kuwa, kwenye makubaliano yao, Bw Mbogo atapewa nafasi ya kuwa na usemi, kinyume na manaibu gavana ambao kwa kawaida wamekuwa kimya.

“Wamekubaliana kwa hali ya kujitolea. Katika ugawaji wa mamlaka, gavana Sonko atampa msaidizi wake asilimia 60 ya serikali ya Mombasa. Hili si jambo la kawaida. Uhuru na naibu wake walipogawa mamlaka ilikuwa nusu kwa nusu. Nataka nimshukuru gavana Sonko kwa kutokuwa na tamaa,” akasema.

Bw Mbogo akikubali kuwa mgombea mwenza, aliwataka wafuasi wake wasivunjike moyo. Kulingana na yeye, makubaliano hayo yanampendelea kuliko Bw Sonko.

“Maslahi ya watu wa Mombasa ni muhimu zaidi kuliko ya Ali Mbogo. Najua haijakuwa rahisi, hasa kwa wafuasi wetu wa Mombasa. Lakini kama alivyosema kinara wangu, tunaunda serikali ya muungano, ingawa tuko katika chama kimoja. Na iwapo makubaliano haya yataheshimiwa, nitakuwa na sehemu kubwa ya serikali,” akasema.

Kujibwaga kwa Bw Sonko katika kinyang’anyiro cha ugavana kunatarajiwa kubadili siasa za Mombasa, ikizingatiwa siasa zake za ukarimu.

Bw Sonko alianza siasa Nairobi aliposhinda ubunge wa Makadara baada ya kifo cha Bw Dickson Wathika. Mnamo 2013, aliwania na akashinda useneta kupitia chama cha The National Alliance (TNA). Alichaguliwa kuwa gavana mwaka 2017 kupitia chama cha Jubilee, lakini akang’olewa na seneti kabla ya muhula wake kukamilika.

Ushindani mkubwa unatarajiwa kutoka kwa Bw Abdulswamad Nassir (ODM), ambaye wiki jana alikabidhiwa tikiti baada ya mfanyabiashara Suleiman Shahbal kujiondoa. Wengine kwenye kinyang’anyiro hicho ni Bw Hassan Omar (UDA) na Dkt William Kingi (PAA).

  • Tags

You can share this post!

‘Unyongaji’ pesa tatizo kwa uchumi

TAHARIRI: Serikali ijayo izibue mifereji ya pesa kwa kaunti

T L