• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 6:26 PM
TAHARIRI: Serikali ikabili mfumko wa bei za bidhaa kuokoa raia

TAHARIRI: Serikali ikabili mfumko wa bei za bidhaa kuokoa raia

NA MHARIRI

MAPEMA juma hili kumekuwepo mjadala mkali sana katika mitandao ya kijamii huku Wakenya wenye ghadhabu wakiishambulia serikali kwa kutochukua hatua zozote kukabiliana na mfumko wa bei za bidhaa za kimsingi.

Nyingi za lawama zilielekezewa wanasiasa ambao licha ya hali ya maisha kuwa ngumu nchini, wao wanaendelea kuchapa siasa za kusaka nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi unaosubiriwa mwezi Agosti.

Wakenya wana kila sababu ya kuwalaumu wanasiasa kwa sababu kati ya mihimili mitatu ya serikali, miwili inashikiliwa na wanasiasa. Serikali ina nguzo tatu ambazo ni Urais, Bunge na Mahakama.

Urais na bungeni ndiko waliko wanasiasa. Hii ina maana kwamba maamuzi mengi yanayoathiri mustakabali wa nchi kwa namna chanya au hasi hufanywa na wanasiasa.

Kichocheo kikubwa cha mfumko wa bei za bidhaa za msingi nchini Kenya ni ushuru wa kupindukia.

Taifa la Kenya katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki linaongoza kwa ughali wa maisha kutokana na ushuru unaotozwa bidhaa mbalimbali tofauti na mataifa jirani.

Kwa mujibu wa Katiba ya 2010, sasa hivi mapendekezo ya makadirio ya pesa hutolewa na waziri wa Fedha kisha kuletwa bungeni kupigwa msasa.

Bunge lina uwezo wa kufuta, kudumisha au kuongeza mapendekezo kuhusu masuala yote. Ni kutokana na mapendekezo ambapo hatimaye waziri huandaa makadirio ya mwisho ili yaidhinishwe na bunge halafu hatimaye Rais.

Mchakato huu unabainisha mamlaka makubwa waliyonayo wanasiasa katika maamuzi mengi yanayoathiri wananchi.

Kwa sasa bidhaa kama vile mafuta ya kupikia, unga wa sima, mchele, sukari, mboga, nyanya n.k ni ghali mno.

Wakenya wengi wanalala njaa kwa kushindwa kumudu kununua chakula. Zaidi ya hayo wanaoishi mijini wanafaa kugharimia nauli ya kila siku mbali na kodi ya nyumba.

Haya yote yakijumuishwa hali ya maisha inakuwa ngumu kupindukia.

Katika sekta ya Kilimo, mwaka huu utaingia katika historia kwa kuwa mwaka ambapo bei za pembejeo zimepanda maradufu.

Mbolea mfuko wa kilo 50 huuzwa kwa Sh6,000 kutoka kwa Sh3,000 mwaka 2021.

Litakuwa kosa kubwa kwa serikali kutoa kipau mbele kwa miundomsingi ilhali raia wake hawawezi kumudu chakula.

Rais akiwa na baraza lake la mawaziri pamoja na bunge wachukue hatua za dhati mapema kukabiliana na mfumko wa bei za bidhaa msingi kabla ya Wakenya kukata tamaa.

Hasira ya umma wenye njaa ni bomu ambalo likilipuka linaweza kusambaratisha taifa.

Serikali isifanye ajizi, ichukue hatua si kesho bali leo kama njia ya kuonyesha kwamba inajali.

You can share this post!

Urusi yashutumiwa kwa ‘kulinda’ waasi

Meja acheka na nyavu mara mbili kuisaidia AIK kutoka sare...

T L