• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
TAHARIRI: Serikali ipige jeki wakulima kumaliza njaa

TAHARIRI: Serikali ipige jeki wakulima kumaliza njaa

NA MHARIRI

KAMATI ya kitaifa inayoshughulikia kiangazi imetoa tangazo ambalo linadidimiza matumaini ya nchi kupata afueni katika siku chache zijazo.

Inasema kwamba mvua fupi zinazonyesha hazitasaidia kumaliza ukame unaoikumba nchi, na kwamba hali hiyo huenda ikadumu kwa zaidi ya mwaka mmoja ujao.

Habari hiyo ya kuvunja moyo inajiri wakati ambapo zaidi ya wakati 300,000 wanahitaji chakula cha msaada Kaunti ya Marsabit.

Mamlaka ya Kitaifa ya Kukabili Kiangazi (NDMA) inasema kuna wakazi 252,882 wanaotegemea wahisani, mashirika ya kijamii na serikali kuwapa chakula.

Wakati hali hiyo ikitarajiwa kuzidi kuwa mbaya kipindi hiki cha Januari, shirika la Msalaba Mwekundu limethibitisha viwango vya utapiamlo miongoni mwa watoto na watu wazima kuwa asilimia 53. Hiki ni kiwango cha juu kote barani Afrika.

Mbali na Marsabit, kaunti za Kwale, Samburu, Kilifi, Kitui na Meru zinakumbwa na hali sawa na hiyo.

Katika maeneo yanayotegemewa kukuza chakula, kuna ripoti za kuenea kwa wadudu viwavi-jeshi. Wadudu hao waharibifu wamezagaa kwenye mashamba kaunti za Kiambu, Muranga na Kirinyaga. Wadudu hawa humaliza ekari za shamba kwa saa chache wasipokabiliwa.

Iwapo watasambaa kwenye mashamba yanayotegemewa kukuza chakula cha kupunguza gharama ya maisha, huenda serikali ikashindwa kutimiza ahadi yake ya kushukisha bei za bidhaa.

Takwimu hizi zote zinaashiria jambo moja; kwamba serikali ya kitaifa na serikali za kaunti, zinapaswa kushirikiana kuweka mikakati ya kuwaepushia raia mateso yanayotokana na athari za kingazi.

Katika maeneo kunakonyesha, wakazi yafaa wahamasishwe na kusaidiwa kukinga na kuhifadhi maji ya mvua kwa matumizi ya mifugo na mashambani mwao.

Kaunti ziunde ushirikiano wa kununua chakula kwa bei nafuu kutoka kaunti jirani zilizo na akiba ya chakula.

Kaunti pia zinaweza kutafuta soko la mifugo au kukuza nyasi kwa gharama ya chini ili wafugaji wapate cha kulisha wanyama wao.

Serikali kupitia wizara ya Kilimo iwanusuru wakulima kwa kuwapelekea maafisa wa nyanjani, wanyunyize dawa za kuangamiza viwavi-jeshi. Hatua ya kuwapa wakulima mbolea ya bei nafuu pamoja na mbegu zilizoidhinishwa ni nzuri.

Kwa vile wakulima hao wametia juhudi na kuanza kukuza chakula, itakuwa vizuri kama juhudi zao zitapigwa jeki kwa kusaidiwa kumaliza wadudu waharibifu.

Hii ndiyo njia pekee ya kuihakikishia nchi kwamba, ifikapo Oktoba au Disemba mwaka huu, kweli kutakuwa na chakula tele.

Hapo, serikali itakuwa imetimiza lengo la kupunguza bei ya bidhaa muhimu, inayochangia gharama ya maisha kuendelea kuwa juu.

  • Tags

You can share this post!

Mwanaume adaiwa kunyofolewa nyeti na mkewe kufuatia ugomvi

Mikakati ya Ruto kumaliza Azimio

T L