• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 6:50 AM
Mikakati ya Ruto kumaliza Azimio

Mikakati ya Ruto kumaliza Azimio

Huku Rais mstaafu Uhuru Kenyatta akitarajiwa kujiuzulu kama mwenyekiti wa Baraza Simamizi la Azimio, mikakati ya Kenya Kwanza itakuwa rahisi kutekeleza kumaliza muungano huo wa upinzani.

Washirika wakuu wa Azimio walitarajiwa kuwa chama cha Jubilee cha Bw Kenyatta na ODM cha aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga ambaye alikuwa mgombea urais wa muungano huo wa upinzani.

Kujiuzulu kwa Bw Kenyatta kutaacha hatima ya Jubilee katika Azimio ikining’inia.

Tayari Azimio inatikiswa na dhoruba ya ndani, washirika wa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka wakimtaka atangazwe kinara wa upinzani na mgombea urais wake kwenye uchaguzi mkuu wa 2027.

Japo Rais William Ruto amesisitiza kuwa anatambua na kuheshimu upinzani muungano tawala umekuwa ukiendelea na mikakati ya kuufifisha upinzani hasa katika maeneo ya Mlima Kenya ambako Naibu Rais Rigathi Gachagua ameapa kuunganisha viongozi wote.

Bw Gachagua amepiga hatua kubwa katika azma hii na baadhi ya vigogo wa Azimio kutoka Mlima Kenya akiwemo aliyekuwa mbunge wa Kieni, Bw Kanini Kega wamemtambua kama msemaji wa eneo hilo.

Bw Kega ambaye ni mkurugenzi wa uchaguzi wa chama cha Jubilee alikuwa sura ya Azimio eneo la Mlima Kenya kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Bw Gachagua alikuwa ameweka makataa ya Desemba 31, 2022 kuunganisha viongozi wa Azimio nyuma ya serikali ya Kenya Kwanza na duru zinasema baadhi ya wanasiasa wa upinzani katika eneo hilo wanasubiri Bw Kenyatta kujiuzulu katika muungano huo ili wauhame.

“Kufikia Desemba mwaka huu (2022) tutakuwa tumemalizana na Azimio eneo hili ili tuweze kukumbatia maendeleo. Nimezungumza na wengi wao na wakaniambia walitishwa na kulazimishwa kujiunga na Azimio lakini wako tayari kuhama,” Bw Gachagua alisema akiwa Nyeri mwaka 2022.

Wazee wa jamii ya Gikuyu ambao walikuwa wakimuunga Bw Odinga wakiongozwa na mwenyekiti na Dkt David Muthoga wametema Azimio na kuungana serikali.

“Kama Baraza la Wazee wa Gikuyu, tunaunga serikali iliyo mamlakani inayoongozwa na Rais Ruto. Hatuna chaguo kwa kuwa ndiye rais wetu, kwa hakika, hatupaswi kushawishiwa kuunga Dkt Ruto na Bw Gachagua,” Bw Muthoga alisema walipomtembelea Gavana Mutahi Kahiga wa Nyeri, mwandani wa Bw Gachagua.

Kenya Kwanza pia imepenya katika ngome za Azimio za Magharibi ya Kenya na Pwani ambako vigogo wa upinzani kama vile Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu) Francis Atwoli amesameheana na Rais Ruto.

Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi amekuwa akiendeleza kampeni ya kurai wanasiasa wa Azimio kujiunga na serikali.

Tayari, magavana wengi wa Azimio, wakiwemo waliochukuliwa kuwa wandani wa karibu wa Bw Odinga na Bw Musyoka, wametangaza uaminifu wao kwa Rais Ruto na kuahidi kushirikiana na serikali yake.

Naibu Mwenyekiti wa Wiper Mutula Kilonzo Jnr anasema kwamba katika mazingira ya sasa ya kisiasa, itakuwa vigumu Azimio kudumu.

“Binafsi sioni Azimio ikidumu, Rais mstaafu ndiye aliiunganisha na kuondoka kwake pamoja na kushindwa na Kenya Kwanza uchaguzini, Azimio itakufa,” Bw Kilonzo aliambia Taifa Leo.

Ripoti za JAMES MURIMI, JUSTUS OCHIENG na BENSON MATHEKA

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali ipige jeki wakulima kumaliza njaa

Ashtakiwa kwa kumlaghai mtaalamu wa masuala ya fedha nchini...

T L