• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 PM
TAHARIRI: Serikali na kampuni zitoe ajira kwa chipukizi wenye vipaji

TAHARIRI: Serikali na kampuni zitoe ajira kwa chipukizi wenye vipaji

NA MHARIRI

UKOSEFU wa ajira ni mojawapo ya matatizo yanayokumba si tu taifa la Kenya bali bara zima la Afrika na maeneo mengi ulimwenguni.

Tatizo hili limesababisha vijana kutamauka hasa kwa kukosa mwelekeo katika maisha siku za usoni. Vijana wetu waliopata elimu kwa kuhitimu vyema vyuoni wamelazimika kuvumilia ahadi kila mara za viongozi kwamba wataimarisha uchumi ili waweze kubuni nafasi za kazi au kuwawezesha kujiajiri kupitia ubunifu wao katika biashara, kilimo au huduma zingine aina ainati katika ekta ya ufundi na teknolojia kwa jumla.

Kando na kundi hili la vijana waliohitimu katika taaluma tofauti tofauti, kuna aina ya chipukizi wengine ambao wamebobea katika fani ya spoti humu nchini. Hawa ni barobaro ambao wamedhihirisha kwamba wana vipawa na talanta za aina yake katika michezo kama vile riadha, soka, raga na uendeshaji magari . Wakati mwingine kundi hili la vijana huwa hawana elimu ya juu ila wana vipaji ambavyo ni adimu.

Mbali na kukuza vipawa vya vijana hawa, serikali inafaa kubuni mikakati ya kuwatafutia ajira zinazoendana na uwezo wao.

Katika dunia ya sasa hasa maeneo ya bara Ulaya na Amerika, wanamichezo wengi chipukizi wamefaidi mno kwa mapato ya hali ya juu kupitia michezo hasa soka, tenisi, riadha na kadhalika.

Ni vyema nchi ya Kenya kuiga mataifa haya kwa kushauri makampuni na mashirika mbalimbali ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali kuwaajiri vijana kama hawa kwenye taasisi hizo.

Kama ilivyo kwa sasa kuna kampuni kadha kama vile Equity Bank, KCB, Tusker na zingine ambazo zimetoa ajira kwa vijana wetu.

Baadhi yao huchezea klabu za mashirika haya huku wakiwa wametengewa majukumu fulani kama kazi ya afisi.

Katika upande wa serikali, Idara ya Ulinzi (KDF) imewafaa vijana wetu pakubwa. Mmoja wao ni mwanasoka Boniface Muchiri aliyechezea klabu ya Tusker kabla kujiunga na timu ya soka ya wanajeshi.

Ingawa ilidaiwa mwanasoka wa Tusker FC Patrick Matasi alikuwa ameahidiwa nafasi ya kazi katika Huduma ya Polisi , ndoto yake haikutimia baada ya klabu hiyo kutomwachilia.

Kuna tetesi za hivi majuzi kwamba mwanadada staa wa soka KingLady Oriyo aliyechezea Zetech Sparks sasa anaelekea klabu ya Ulinzi Starlets ambao watampa ajira katika KDF. Hatua kama hizi ni za kutia moyo vijana wetu na hazina budi kuigwa na mashirika mengine.

You can share this post!

Azimio wamsuta Rais kwa kukwepa suala la vita dhidi ya...

Kocha Jurgen Klopp atetea beki Alexander-Arnold baada ya...

T L