• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Kocha Jurgen Klopp atetea beki Alexander-Arnold baada ya kupuuzwa na mkufunzi wa timu ya taifa ya Uingereza

Kocha Jurgen Klopp atetea beki Alexander-Arnold baada ya kupuuzwa na mkufunzi wa timu ya taifa ya Uingereza

Na MASHIRIKA

KOCHA Jurgen Klopp wa Liverpool amesema hatawahi kumtema Trent Alexander-Arnold katika kikosi cha kwanza cha timu yake licha ya beki huyo kupuuzwa na mkufunzi wa Uingereza, Gareth Southgate.

Alexander-Arnold, 23, hakuwajibishwa na Southgate dhidi ya Italia na akatemwa kwenye kikosi kilichovaana na Ujerumani katika michuano miwili iliyopita ya kimataifa iliyotandazwa na Uingereza. Walicharazwa na Italia 1-0 kabla ya Ujerumani kuwalazimishia sare ya 3-3 katika mechi hizo za Uefa Nations League.

Ingawa Klopp ametaka Alexander-Arnold kuimarisha ujuzi wa kukabili wapinzani, amekiri kuwa ubora wa nyota huyo kikosini hudhihirika zaidi kila anapocheza kwa kuvamia.

“Bila shaka maamuzi yangu yangekuwa tofauti. Lakini tatizo ni kuwa sidhibiti mikoba ya Uingereza. Kuteua Alexander-Arnold kuingia katika kikosi cha kwanza si maamuzi magumu kwa kocha yeyote kufanya. Ni beki wa haiba kubwa ambaye nitamsajili katika klabu yoyote nitakayonoa baada ya Liverpool,” akasema Klopp.

Southgate kwa upande wake amesisitiza kuwa mchezo wa Alexander-Arnold kwa sasa uko chini ukilinganishwa na wa difenda Kieran Trippier ambaye hushirikiana vyema zaidi na Reece James katika safu ya ulinzi ya Uingereza.

Alexander-Arnold aliyekosa kipute cha Euro 2020 kutokana na jeraha, amechezea Uingereza mara moja pekee mwaka huu. Hata hivyo, amekuwa tegemeo la Liverpool huku akisaidia miamba hao kutwaa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) katika kipindi cha miaka michache iliyopita.

Japo anatamba katika ngazi ya klabu, ameshindwa kuhamisha fomu hiyo kwenye soka ya kimataifa na amechezea Uingereza mara 17 pekee tangu avalie jezi za kikosi hicho kwa mara ya kwanza tangu 2018.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali na kampuni zitoe ajira kwa chipukizi...

Ebola: Hofu raia wa Kenya akishukiwa

T L