• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:50 AM
Azimio wamsuta Rais kwa kukwepa suala la vita dhidi ya ufisadi

Azimio wamsuta Rais kwa kukwepa suala la vita dhidi ya ufisadi

WABUNGE wa upinzani wamekosoa Rais William Ruto wakidai alikosa kuangazia mikakati ya serikali yake kuhusu vita dhidi ya ufisadi kwenye hotuba yake bungeni jana Alhamisi.

Wakiongozwa na kiongozi wa Wengi, Bw Opiyo Wandayi, wabunge hao wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya pia walisema kuwa hotuba hiyo iliacha nje masuala mengine yanayowahusu Wakenya.

“Kwangu kama kiongozi wa mrengo wa Azimio katika bunge hili, sioni lolote lenye thamani katika hotuba hii kwa sababu haikuangazia vita dhidi ya ufisadi. Hii ni kwa sababu jinamizi hili ndilo changamoto kubwa kwa ustawi wa kiuchumi wa taifa hili,” akasema Bw Wandayi, ambaye ni Mbunge wa Ugunja.

“Rais atapata wapi Sh50 bilioni za kuwekeza kwenye Hazina ya Hasla ilhali hajatoa mwongozo kuhusu namna atakavyookoa jumla ya Sh600 bilioni ambazo huibwa kupitia sakata za ufisadi kila mwaka nchini?” akauliza mbunge huyo ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC) katika Bunge la 12.

Kwa upande wake, Junet Mohamed alilalamika kuwa hotuba ya Rais ilikuwa fupi zaidi kiasi kwamba haikuangazia jinsi atapambana na kero la kupanda kwa bei ya bidhaa za kimsingi kama vile mafuta.

“Ukweli ni kwamba hotuba ya Rais imewavunja moyo Wakenya. Hajasema ni lini bei ya unga itashuka hadi Sh100; hajasema ni lini bei ya mafuta itashuka, miongoni mwa ahadi nyingine alizotoa kwa Wakenya,” akasema mbunge huyo wa Suna Mashariki.

Bw Mohammed alidai kuwa Rais Ruto alikuwa akiongea kana kwamba angali katika kampeni kwani alitumia muda mwingi kutoa ahadi zaidi.

“Ninashangaa kuwa bado anazungumza kuhusu mahasla na “bottom up” katika idara ya mahakama. Aidha, anatoa ahadi ya mpya ya kutekeleza mageuzi katika NSSF (Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni) ilhali hajatimiza mengi aliyowaahidi Wakenya,” akasema.

Wengine waliokosoa hotuba ya rais walikuwa maseneta Ledama Ole Kina (Narok) na Godffrey Osotsi (Vihiga).

Lakini wabunge wa mrengo wa Kenya Kwanza walisifu hotuba ya Rais Ruto.

Wengine tuliozungumza nao katika majengo ya bunge walielezea kufurahishwa na wito wake wa kutaka hazina ya ustawi wa maeneo bunge (CDF) idumishwe.

“Rais alifanya vizuri kwa kutoa hotuba fupi na ambayo Wakenya wataielewa kwa haraka. Ameangazia masuala yote yanayowahusu Wakenya haswa gharama ya maisha kwa kusema serikali itapunguza bei ya mbolea zaidi kuliko bei ya sasa ya Sh3,500,” akasema Mbunge wa Emuhaya Omboko Milemba (ANC).

  • Tags

You can share this post!

Ruto abuni mbinu za raia kujitajirisha

TAHARIRI: Serikali na kampuni zitoe ajira kwa chipukizi...

T L