• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
TAHARIRI: Si lazima serikali itimize masharti yote ya shirika la kifedha la IMF

TAHARIRI: Si lazima serikali itimize masharti yote ya shirika la kifedha la IMF

NA MHARIRI

KATIKA miaka ya hivi majuzi, Shirika la Kimataifa la Kifedha (IMF) limekuwa likitoa masharti makali ya kifedha linayotaka Kenya iyafuate ndipo ifaulu kupewa mikopo.

Miongoni mwa masharti hayo ni kuhakikisha kuwa mipango yote ya ruzuku na ufadhili kwa mashirika mbalimbali ya umma, inafutiliwa mbali, na kuongeza ushuru wa bidhaa mbalimbali.

Bei ya umeme pia imepanda maradufu.

Serikali ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta iliyapuuza mengi ya masharti ya shirika hilo, lakini utawala mpya wa Kenya Kwanza chini ya uongozi wa Rais William Ruto umeonyesha kila ishara kuwa utayakumbatia masharti hayo yote kwa dhamira ya kupewa mikopo.

Miongoni mwa masharti hayo ambayo Serikali ya Ruto imeanza kutekeleza ni kuondoa ruzuku ya mafuta ya petroli, ruzuku ya unga wa mahindi na ufadhili wa vyuo vikuu.

Hata ingawa waziri wa Elimu, Ezekiel Machogu jana Jumanne alighairi dhamira yake ya kuondoa ufadhili wa vyuo vikuu, tayari kauli yake kuwa serikali inapanga kukatiza ufadhili huo inafasiriwa kama ishara tosha kuwa serikali ya Rais Ruto haitasita kuchukua hatua yoyote ndipo ikubalike machoni pa IMF, hata kama hatua hiyo itaathiri raia wa kawaida ambaye kwa sasa anaumia sana kutokana na mzigo mkubwa wa gharama ya maisha.

Baada ya kuondoa ruzuku ya mafuta, japo kwa nusu, kwa sasa lita moja ya petroli inauzwa kwa angaa Sh179. Iwapo ruzuku nzima itafutwa, basi Mkenya atanunua bidhaa hiyo kwa Sh215.

Hilo litakuwa ongezeko la takribani Sh60 ukilinganisha na bei ya kawi hiyo muhimu wakati wa utawala wa Bw Kenyatta.

Nyongeza hiyo bila shaka imepaliza gharama ya maisha maadamu shughuli nyingi za kiuchumi hasa usafiri huendeshwa na kawi hiyo.

Hii ni mbali na gharama ya uzalishaji viwandani kupaa baada ya bei ya umeme kuzidishwa kwa karibu mara mbili.

Kwa upande wa vyuo vikuu, Serikali imekuwa ikidhamini kila mwanafunzi kwa Sh70,000 kwa mwaka. Hivyo basi kuondolewa kwa ufadhili huo kuna maana kuwa mzigo huo utamrudia mwanafunzi.

Hakika Wakenya wengi hawataweza kumudu karo kiasi hicho hasa inapozingatiwa kuwa hata ada inayotozwa sasa ya Sh16,000 huwashinda wengi wa wanafunzi.

Kutekelezwa kwa hatua hiyo, kwa hivyo, kutawafungia nje wanafunzi wengi werevu wasiokuwa na uwezo.

Hakika, masharti ya IMF yatamuumiza zaidi Mkenya wa kawaida iwapo serikali haitayafumbia mengi yayo macho kwa kusudi la kumpunguzia Mkenya madhila anayopitia kwa sasa.

You can share this post!

Wizara yampa Mudavadi uskwota ofisi zake zikifanyiwa...

Je, wajua chakula huathiri afya yako ya akili?

T L