• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 4:39 PM
TAHARIRI: Tuwe makini zaidi kukabili mabadiliko ya tabianchi

TAHARIRI: Tuwe makini zaidi kukabili mabadiliko ya tabianchi

NA MHARIRI

DALILI zinazidi kuonyesha kuwa tusipomakinika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, tutazidi kujuta kadri na jinsi miaka inavyosonga.

Mwaka huu 2023, tayari inahofiwa kutakuwa na msimu mwingine wa kiangazi cha muda mrefu.

Mamilioni ya Wakenya wameteseka kwa miaka minne iliyopita kwa sababu ya kiangazi.

Kila mwaka, mvua inayotarajiwa huwa hainyeshi kwa kiwango cha kawaida.

Kiasi kidogo mno cha mvua ambayo hata haionekani kabisa katika baadhi ya maeneo ya nchi, hakiwezi kuendelea kutegemewa kuzalisha chakula cha kutosheleza mahitaji ya nchi nzima.

Wananchi wengi wanataabika kwa njaa kwani ardhi ziko kavu, na mifugo wanaangamia kwa kukosa lishe na maji ya kutosha.

Katika miaka iliyopita, kulikuwa na maonyo kutoka kwa wataalamu mbalimbali wa mazingira kuhusu hatari iliyotukodolea macho lakini wengi wakapuuza.

Sio Kenya pekee, bali ulimwenguni kote, binadamu waliendelea na tabia mbovu za kukata miti kiholela na kuendeleza shughuli zisizofaa katika vyanzo vya maji.

Viwanda vilikubaliwa kuchafua mazingira, iwe ni hewani au majini kwa viwango vya kutamausha.
Haya yote yamesababisha mabadiliko ya tabianchi ambapo tumeona mito na maziwa yakikauka na kuacha jamii nyingi mashakani.

Wakati huu, kuna wengi ambao wanatamani kujitosa katika upandaji wa miti ili kujaribu kurudishia mazingira hali yake ya zamani, lakini imekuwa taabu.

Upandaji miti unahitaji mvua au angalau maji ya kunyunyizwa, lakini hayo maji hayapatikani katika sehemu zinazohitaji kurudishiwa miti zaidi.

Taifa hili litalazimika kutafakari kwa kina kuhusu hatua mwafaka zinazoweza kuchukuliwa ili kuokoa vizazi vijavyo.
Ikiwa hali itaachwa iendelee jinsi ilivyo, kuna hatari kubwa inayotusubiri katika enzi zijazo.

Wadau wote wanaohusika na masuala ya mazingira pamoja na kila mwananchi, ajitwike jukumu la kutathmini hatua zinazofaa kutekelezwa kwa dharura ili kuepusha madhara tunayoshuhudia kuendelea kuzidi.

Serikali, kwa njia ya uaminifu, iweke rasilimali za kutosha kutekeleza miradi ya kutunza mazingira.

Mbali na hayo, kuwe pia na rasilimali za kutosha kuepushia wananchi hasara zaidi ya zile wanazoendelea kupata kutokana na uharibifu wa mazingira.

  • Tags

You can share this post!

Hali ngumu ya maisha Siku ya Wapendanao ikiadhimishwa

CHARLES WASONGA: Uhuru asinyimwe pensheni kwa kujihusisha...

T L