• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:55 PM
CHARLES WASONGA: Uhuru asinyimwe pensheni kwa kujihusisha na siasa

CHARLES WASONGA: Uhuru asinyimwe pensheni kwa kujihusisha na siasa

NA CHARLES WASONGA

RAIS mstaafu Uhuru Kenyatta sasa ni raia wa kawaida japo anayeheshimika kama rais wa nne wa Jamhuri ya Kenya.

Kama Wakenya wengine, Bw Kenyatta yuko huru kufurahia haki zake zote za kisiasa zilizoorodheshwa katika kipengele cha 38 cha Katiba ya sasa.

Lakini kulingana na Sehemu 4 ya Sheria Kuhusu Malipo ya Pesheni ya Rais, Bw Kenyatta anaweza kupokonywa malipo hayo ikiwa ataendelea kujihusisha na siasa. Sehemu hiyo ya sheria, hata haijaelezea ni namna gani rais mstaafu atakavyojihusisha na siasa kiasi cha kufikia hatua ya kunyimwa malipo ya pensheni yake.

Aidha, sehemu ya 6 (1) ya sheria hiyo inasema kuwa rais mstaafu hapaswi kushikilia wadhifa wa uongozi katika chama au muungano wowote wa kisiasa miezi sita baada ya kuondoka rasmi afisini.

Bw Kenyatta aliondoka afisini mnamo Septemba 13, 2022 baada ya kumkabidhi Rais wa sasa William Ruto, hatamu za uongozi wa taifa hili kwa miaka mitano ijayo.

Kwa hivyo, kwa mujibu wa sheria hii, Bw Kenyatta anahitajika kujiuzulu kama kiongozi wa chama cha Jubilee, na mwenyekiti wa baraza kuu la muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, mnamo Machi 13, 2023.

Akiongea mjini Luanda, Kaunti ya Vihiga, Bw Kenyatta alitangaza wazi kwamba japo amestaafu kama Rais, ataendelea kujihusisha na siasa “kwani ni haki yangu ya kikatiba”.

Aidha, alikariri kuwa angali anamtambua Raila Odinga kama kiongozi wake, kisiasa, na kwamba bado anamuunga mkono alivyofanya katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2022.

Kwa hivyo, kwa mtazamo wangu, Bw Kenyatta hajafanya kosa lolote kwa kusema kuwa ataendelea kujihusisha na siasa, sawa na kumuunga mkono Bw Raila.

Hii ndiyo maana sikubaliani na wabunge na maseneta wa Kenya Kwanza wanaoitaka serikali imnyime Bw Kenyatta malipo yake ya pensheni kwa msingi kuwa anaendelea kujihusisha na siasa.

Wakiongozwa na kiongozi wa wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot, wanasiasa hao wanadai kuwa kwa kujihusisha na siasa, Bw Kenyatta anaonyesha kuwa anamdharau na hamtambui Dkt Ruto kama Rais wa Jamhuri ya Kenya.

Ningependa kuwakumbusha wanasiasa hao kwamba Bw Kenyatta anamtambua Dkt Ruto kama mshindi katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2022.

Hii ndiyo maana licha ya kwamba alimuunga mkono Bw Odinga katika kinyang’anyiro hicho, alimpokeza rasmi Dkt Ruto mamlaka Septemba 13, 2022 katika uwanja wa michezo wa Kasarani.

Wakati huu Bw Kenyatta anapaswa kupokea pensheni ya Sh700 milioni mbali na manufaa mengine kama vile marupurupu ya nyumba, walinzi, wafanyakazi wa nyumba, magari ya serikali miongoni mwa mafao mengine yanayotokana na pesa za umma.

Kwa hivyo, serikali haifai kumyima Bw Kenyatta pensheni yake kwa msingi kuwa anajihusisha na siasa baada ya kustaafu kama rais.

Hii ni kwa sababu licha ya kuwa rais mstaafu, Bw Kenyatta hajapokonywa haki ya kuwa mwanachama wa chama cha kisiasa, haki ya kupiga kura, na haki ya kumuunga mgombeaji urais yeyote katika chaguzi kuu zijazo.

Kiongozi huyo bado anafurahia haki zote za kisiasa kwa mujibu wa kipengele cha 38 cha Katiba.

Sheria kuhusu Pensheni ya Rais haiwezi kutumiwa kama sababu ya kumnyima Bw Kenyatta kile ambacho ni haki yake.

Sheria hii haiwezi kuwa na nguvu kuliko kifungu au kipengele chochote cha Katiba.

Hii ni kwa sababu kulingana na kipengele cha 2 cha Katiba hii, endapo sheria yoyote itakinzana na kipengele chochote cha katiba hii, hitaji la katiba ndilo litazingatiwa.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Tuwe makini zaidi kukabili mabadiliko ya tabianchi

BENSON MATHEKA: Ni hatari kuu Bunge kupoteza uhuru wake wa...

T L