• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Uamuzi wa kufunga shule ghafla hakika utatatiza wengi

TAHARIRI: Uamuzi wa kufunga shule ghafla hakika utatatiza wengi

NA MHARIRI

UAMUZI wa Wizara ya Elimu kutangaza ghafla kwamba shule zifungwe leo Jumanne, unaashiria uwezekano wa kuwa kuna ukosefu wa mipangilio bora kuhusu maandalizi ya Uchaguzi Mkuu.

Uchaguzi Mkuu katika taifa lolote lile huwa ni shughuli ambayo haifai kamwe kuachiwa idara moja au mbili pekee.

Hii ni kutokana na kuwa, shughuli hiyo nzima inahitaji mchango na ushirikiano kikamilifu kutoka kwa idara mbalimbali za kiserikali na pia za kibinafsi ili kufanikisha uchaguzi kwa njia isiyo na matatizo yoyote.

Kufikia sasa, tumekuwa tukiona maandalizi mengi yakihusisha idara za usalama na teknolojia za mawasiliano, mbali na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ambayo ndiyo mwandalizi mkuu.

Awali, ilikuwa imepangiwa kwamba shule zifungwe ifikapo Ijumaa ili kufanikisha maandalizi ya uchaguzi wa wiki ijayo.

Katika miaka yote huwa inafahamika kuwa, shule ndizo hutumiwa sana kama vituo vya uchaguzi.

Kwa msingi huu, ingetarajiwa kwamba mipango yote ingefanywa mapema kuhusu wakati ambapo wanafunzi, walimu na wafanyakazi wengine watatakikana kuondoka shuleni ili kutoa nafasi kwa maandalizi.

Hakika, matarajio kwamba maandalizi yote yangekamilika kwa njia ipasayo katika kipindi cha siku tatu pekee kuanzia Ijumaa yalikuwa hatari.

Kuna mambo mengi ambayo yanatakikana kufanywa kabla mkesha wa siku ya uchaguzi.

Ni sharti maafisa wa uchaguzi na wadau wengine wakuu wakague baadhi ya sehemu ambazo zitatumiwa kama vituo vya uchaguzi kabla mkesha wa Agosti 9.

Hatua hii ndiyo itatoa nafasi kwao kutambua changamoto zilizopo ili zitatuliwe kwa muda unaofaa.

Ikizingatiwa kwamba chaguzi za Kenya siku hizi zinazingatia sana teknolojia, mojawapo ya mambo muhimu ambayo yanatakikana kukaguliwa kikamilifu ni uwezo wa vituo hivi kupokea mawimbi yenye nguvu za kutosha kwa wapigakura kutekeleza wajibu wao, na vilevile kwa maafisa kutuma matokeo ya uchaguzi bila shida.

Wadau wanaohusika katika maandalizi ya uchaguzi walinoa kwa kusubiri hadi dakika hizi za mwisho kubadilisha siku ambapo shule zinafaa kufungwa.

Kuna wazazi ambao hawakuwa wamejiandaa kwa hali hii, kwa mfano kugharimia usafiri wa watoto wao hivi ghafla, na hivyo basi mipango mengi itavurugwa.

Tusisahau pia kuna watoto ambao ni lazima wakachukuliwe na wazazi au walezi wao shuleni ilhali hapakuwa na mipango hiyo kwa sasa.

You can share this post!

Ruto asihi ngome yake kuwakataa wawaniaji wasio wa chama...

Kenya Kwanza wammezea mate Shahbal

T L