• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Kenya Kwanza wammezea mate Shahbal

Kenya Kwanza wammezea mate Shahbal

VALENTINE OBARA Na WINNIE ATIENO

MUUNGANO wa Kenya Kwanza, umeanza kumrushia mistari mfanyabiashara, Bw Suleiman Shahbal, katika juhudi za mwishomwisho kujiimarisha Mombasa kabla Uchaguzi Mkuu ufanyike wiki ijayo.

Hatua hiyo imejiri baada ya muungano huo kupata uungwaji mkono kutoka kwa aliyekuwa gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko, na Mbunge wa Kisauni, Bw Ali Mbogo, ambao azma yao ya kuwania afisi ya gavana wa Mombasa kupitia Chama cha Wiper ilizimwa.

Akizungumza Jumatatu, mgombeaji ugavana Mombasa kupitia Chama cha UDA, Bw Hassan Omar, alidai mgombea mwenza wake, Bi Selina Maitha, anategemewa kufanikisha mpango wa kumshawishi Bw Shahbal kujiunga nao.

“Hata nimemtuma Selina akaongee na Suleiman Shahbal ili awe na ujasiri kujiunga nasi,” akasema Bw Omar.

Bi Maitha alikuwa ameteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Bw Shahbal, kabla Chama cha ODM kumshawishi mfanyabiashara huyo kumwachia nafasi Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, kuwania urithi wa kiti cha Gavana Hassan Joho katika uchaguzi wa Agosti 9.

Hata hivyo, Bw Shahbal alipuuzilia mbali wazo hilo la Bw Omar.

“Hao wanajidanganya. Ninashikilia imani kwamba ODM inaweza kuokoa nchi hii ndiposa nilibaki ndani ya ODM licha ya yale yaliyotokea. Mimi ni mtu anayechukua msimamo na kuufuata hadi mwisho. Sitabanduka katika Azimio chini ya uongozi wa Baba,” akaambia Taifa Leo.

Wakati huo huo, muungano wa Kenya Kwanza umefuata nyayo za wapinzani wao wa Azimio la Umoja One Kenya, na kumpendekeza mwanasiasa wa Pwani atengewe wadhifa wa waziri wa ardhi endapo Naibu Rais William Ruto, atashinda urais kupitia Chama cha UDA wiki ijayo.

Bw Mbogo, amefichua kuwa ameahidiwa wadhifa huo baada ya kujiunga na mrengo huo mwishoni mwa wiki iliyopita.

Miezi michache iliyopita, kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, anayewania urais kupitia kwa Azimio, alimpendekeza Bw Joho, kuwa waziri wa ardhi endapo mrengo wake utafanikiwa kushinda urais katika uchaguzi wa Agosti 9.

Wanasiasa wa Kenya Kwanza walikuwa wamepuuzilia mbali hatua hiyo na kusema changamoto za ardhi zinazokumba Pwani hazitegemei waziri kuchaguliwa kutoka eneo hilo, bali kuwepo kwa mifumo bora ya kusimamia sekta ya ardhi.

“Baina ya Joho kama waziri wa ardhi na mheshimiwa Ali Mbogo, ni nani mnamwamini zaidi? Ni nani mna imani atatatua tatizo la uskwota? Mimi sitanyakua shamba la mtu,” akasema Bw Mbogo, katika kampeni Jumapili jioni.

Chama cha Wiper kilijitenga na hatua ya Bw Sonko na kusema imethibitisha alikuwa katika mrengo wa Dkt Ruto wakati wote ila akajifanya kuwa katika Azimio.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Uamuzi wa kufunga shule ghafla hakika utatatiza...

Magoha ashangaza kufunga shule ghafla

T L