• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 4:47 PM
TAHARIRI: Ucheleweshaji wa malipo ya wakandarasi ukomeshwe

TAHARIRI: Ucheleweshaji wa malipo ya wakandarasi ukomeshwe

NA MHARIRI

INASIKITISHA kuwa baadhi ya Wakenya waliosambazia serikali bidhaa au kutoa huduma wamekufa kutokana na hasa tatizo la kimawazo au hali duni ya maisha baada ya serikali kuchelewa kuwalipa haki yao.

Wiki jana ilibainika kuwa Wakenya wanadai serikali ya kitaifa na kaunti pamoja na mashirika ya kiserikali zaidi ya Sh480 bilioni kwa jumla.

Baadhi ya wakandarasi wamejipata katika hali ambapo milki zao zinapigwa mnada baada ya kuchukua mikopo kwenye benki na mashirika mengine ya kifedha kisha wakashindwa kulipa baada ya kucheleweshewa malipo yao na serikali mashirika hayo ya kiserikali.

Tatizo hili ni kubwa kiasi kwamba baadhi ya wazazi na walezi wameshindwa kuwapeleka watoto wao shuleni kwa kukosa karo. Wamekosa karo baada ya serikali kuchelewesha, tena kwa muda mrefu, malipo yao.

Wahasiriwa wengi wamecheleweshewa malipo yao kwa zaidi ya mwaka mmoja, wengine miezi sita na wengine mitatu.

Ifahamike kuwa mjasiriamali anapopewa kandarasi na shirika au kampuni yoyote ile, aghalabu huwa hana pesa za kutosha kukamilisha mradi huo.

Hali hiyo humsukuma katika mashirika ya kukopesha ili apate pesa za kukamilishia mradi husika akijua atalipwa halafu arejeshe mkopo naye abaki na faida ya kujisukumia mbele.

Malipo hayo yanapolimatia, basi mjasiriamali huyo hujipata kwenye mtaanziko mkubwa ikiwemo mzongo wa mawazo, hatari ya mali kunadiwa na kushindwa kumudu mahitaji ya kimsingi ya familia yake.

Kwa njia hiyo mtu anayefaa kusaidiwa kujiinua kimaisha, ‘husaidiwa’ na shirika lililoagiza bidhaa au huduma zake kuanguka.

Tukio kama hilo si zuri kwa taifa linalojitahidi kuinua uchumi wake na wa raia wake.

Sharti serikali ya Kenya Kwanza ianze upesi kuwazia suala la kulipa madeni haya katika muda mfupi.

Maadamu tatizo hili limekita sana katika serikali za kaunti, Hazina ya Kitaifa ijizatiti kutuma mgao unaofaa kwa kaunti kwa haraka.

Kaunti zimelalamika kuwa tatizo la kuwalipa wakandarasi hao huwa ni ucheleweshaji wa serikali kuu katika kutuma mgao unaotosha .

Zinasema aghalabu mgao unaotumwa hutosha tu mishahara na marupurupu bali si maendeleo.

Hali hii inafaa iwakoseshe usingizi watunga sera wa serikali ya Dkt Ruto.

Aidha, sheria inayolazimisha mashirika hayo kutoa pesa kwa haraka inafaa iimarishwe ili kuondoa ucheleweshaji huo. Sheria hiyo itoe adhabu kwa yeyote anayechelewesha malipo.

  • Tags

You can share this post!

Mahakama yafuta ushindi wa mbunge wa Magarini Harrison Kombe

Safari ya kisiasa ya Harrison Kombe ambaye mahakama imefuta...

T L