• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 1:02 PM
TAHARIRI: Umekuwa msimu wa Ligi Kuu yenye pandashuka tele

TAHARIRI: Umekuwa msimu wa Ligi Kuu yenye pandashuka tele

NA MHARIRI

KWA mara ya mwisho msimu huu timu za Ligi Kuu ya Soka (KPL) zitashuka dimbani kusakata mechi za kufunga msimu.

Umekuwa msimu wa mihemko na pandashuka za kila aina katika usimamizi wa soka nchini.

Cha kusononesha zaidi ni wadhamini wakuu wa soka walipojiondoa msimu ukianza Septemba iliyopita.

Muhula mpya uling’oa nanga ukigubikwa na sintofahamu jinsi ligi itafadhiliwa, baada ya kampuni ya Odibet kuondoa udhamini wake.

Odibet ilitangaza rasmi kuagana na Shirikisho la Soka Nchini (FKF) kwa kile kinachosemekana ni kutoridhishwa na juhudi za shirikisho kukuza soka mashinani.

Kampuni hiyo ilikuwa ikitoa ufadhili wa Sh127 milioni katika mkataba wa miaka mitatu uliotangazwa Desemba 2019.

Ufadhili huo ulikuwa kwa Ligi ya Kitaifa Daraja ya Kwanza, Ligi ya Kitaifa Daraja ya Pili na Ligi ya Kaunti.

Kujiondoa kwa Odibet kulikujia miezi kadha baada ya wafadhili wakuu wa KPL, Betking, kukatiza uhusiano wao na FKF kuelekea mwisho wa msimu uliotangulia.

Betking, kutoka Nigeria, ilikuwa imetoa ufadhili wa Sh1.2 bilioni katika mkataba wa miaka mitano kuanzia Julai 2020.

Nyingi ya timu za KPL zilizokuwa zikitegemea ufadhili huo zilififia, huku Mathare United ikitupwa nje ya ligi kwa kukosa kuwajibikia mechi tatu kwa sababu ya uchafuchefu.

Aidha, vilio vya wanasoka kutolipwa malimbikizo ya mishahara ilishamiri msimu huu. Wengi tu waliendeleza migomo baridi.Kabla kidonda kupoa, wiki chache zilizopita Betika, iliyokuwa ikifadhili Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL), pia ilitangaza kujiondoa.

Minong’ono kwamba pia inawazia kuondoa ufadhili huo wa Sh45 milioni kwa miaka mitatu, ulioanza Novemba 2019, ilikuwa imeshaenea.Ni wazi kwamba wafadhili wa soka humu nchini hawakuwa na imani tena jinsi FKF ilikuwa ikiongozwa.

Hata hivyo, hatua ya serikali kubandua FKF na kuweka Kamati Simamizi, na sasa ya Muda, hazijafua dafu.Matokeo yake ni Kenya kupigwa marufuku na Shirikisho la Soka Duniania (FIFA).Sasa timu ya timu ya taifa Harambee Stars haitashiriki Kombe la Afrika (AFCON) 2023 wala mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia lijalo baada ya Qatar.

Ni matukio ya kushangaza jinsi usimamizi wa soka unavyozidi kudorora kila uchao.Ligi inapofikia tamati kesho Jumapili, wadau watumie likizo inayokuja kutafakari kwa kina – pasipo ubinafsi, ujeuri wala tamaa – jinsi tutavyoiokoa soka yetu.

You can share this post!

Ruto, Raila wahepa marafiki wa karibu

Mkuu wa shule ya msingi kizimbani kwa kupora Sh2 milioni

T L