• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Ruto, Raila wahepa marafiki wa karibu

Ruto, Raila wahepa marafiki wa karibu

NA LEONARD ONYANGO

NAIBU Rais William Ruto na mshindani wake mkuu wa kiti cha urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, Raila Odinga wamewaondoa wandani wao wa muda mrefu katika misafara yao ya kampeni.

Badala yake, wawili hao wamekumbatia wanasiasa kutoka maeneo mengine ambayo si ngome zao za Rift Valley na Nyanza, katika kile wadadisi wanasema ni hatua inayolenga kupatia kampeni zao sura ya kitaifa.

“Naibu Rais akianza kuandamana na wandani wake wa Rift Valley katika maeneo mengine ya nchi atafanya chama chake cha UDA kuonekana kama kinachomilikiwa na watu wa kutoka nyumbani kwake,” anasema Bw Javas Bigambo, mdadisi wa masuala ya kisiasa.

Ni sababu sawa na hiyo ambayo imesababisha Bw Odinga kuhepa wakereketwa wake wa muda mrefu kutoka Nyanza ambao wamekuwa sura ya chama chake cha ODM.

“Bw Odinga anatumia muungano wa Azimio kuwania urais kwa sababu alihofia kuwa chama cha ODM kingemfanya kukosa kura katika baadhi ya maeneo ambako hakina ushawishi kama vile Mlima Kenya. Hivyo, kuzunguka na idadi kubwa ya viongozi ambao wamekuwa wakihusishwa na ODM kwa muda mrefu ni hatari kwa kampeni zake, ndiposa imebidi kutumia wanasiasa kutoka nje ya Nyanza kuongoza kampeni zake,” anasema Bw Bigambo.

Kati ya marafiki wa karibu ambao Dkt Ruto amejitenga nao kwenye kampeni zake za kitaifa ni pamoja na Seneta wa Nandi Samson Cherargei na wabunge Oscar Sudi na Caleb Kositany.

Wakereketwa wake wengine wakiwemo Seneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) na waziri wa zamani Charles Keter wameingizwa kwenye makundi ya kampeni yanayoongozwa na mwaniaji mwenza wake Rigathi Gachagua na Kinara wa ANC Musalia Mudavadi.

Hatua hii imewanyima usemi waliokuwa nao awali katika kampeni za Dkt Ruto.

Badala yake Dkt Ruto amewatwika wanasiasa kutoka nje ya Rift Valley jukumu la kuongoza kampeni zake, ambapo magavana Amason Kingi (Kilifi), Moses Lenolkulal (Samburu) na Alfred Mutua (Machakos), wabunge Moses Kuria (Gatundu Kusini)), Kimani Ichung’wah (Kikuyu), Aden Duale na Peris Tobiko (Kajiado Mashariki) wanatekeleza wajibu mkubwa zaidi.

NYANZA

Kwa upande wake, Bw Odinga katika kampeni zake amekwepa washirika wake wa muda mrefu kutoka Nyanza kama vile Seneta wa Siaya James Orengo na wabunge John Mbadi (Suba Kusini), Opiyo Wandayi (Ugunja), Otiende Amollo (Rarieda), Millie Odhiambo (Suba Kaskazini), Gladys Wanga (Homa Bay) na Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyong’o kati ya wengineo.

Badala yake, Gavana wa Kisii James Ongwae na Mbunge wa Dagoretti Kaskazini Simba Arati, ambaye anawania ugavana wa Kisii kupitia tiketi ya ODM, wametwikwa jukumu la kuongoza kampeni zake katika eneo la Nyanza.

Bw Orengo amejumuishwa katika kikosi cha Nyanza, kumaanisha kuwa hatakuwa akizunguka na Bw Odinga kote nchini kusaka kura za uraisBw Odinga tayari amegawa vikosi vyake katika makundi 16 yakiongozwa na wanasiasa kutoka nje ya ngome yake ya Nyanza.

Kikosi kinachoongozwa na Bw Odinga kinajumuisha mwaniaji mwenza wake Martha Karua, aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth, Naibu Gavana wa Nyeri Caroline Karugu, Bw Wandayi, Mbunge wa Likoni Mishi Mboko na wabunge Maina Kamanda (Maalumu), Kanini Kega (Kieni) na Junet Mohamed (Suna Mashariki).

  • Tags

You can share this post!

Mung’aro aahidi kuongeza bajeti ya sekta ya elimu...

TAHARIRI: Umekuwa msimu wa Ligi Kuu yenye pandashuka tele

T L