• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
TAHARIRI: Utawala wa Jubilee hauna cha kujivunia kuhusu michezo

TAHARIRI: Utawala wa Jubilee hauna cha kujivunia kuhusu michezo

NA MHARIRI

RAIS Uhuru Kenyatta alipopigia debe mafanikio ya utawala wake katika hotuba ya Sikukuu ya Madaraka katika uwanja wa Uhuru Gardens, Nairobi, michezo ilikosekana kwenye orodha hiyo ndefu.

Katika takriban saa nzima ambayo rais alidondosha miradi ya miundomsingi, teknolojia, umeme na afya ambayo utawala wake wa Jubilee umetekeleza, hapakuwa na la kujivunia kuhusu michezo.

Itakumbukwa jinsi wakati wa kampeni za 2007 Bw Kenyatta na naibu wake Dkt William Ruto walivumisha manifesto yao kwa ahadi ya kujenga viwanja vya kisasa vya michezo ili kukuza talanta za spoti na hivyo kuunda nafasi tele za ajira kwa vijana.

Hesabu ya viwanja 47 katika kila kaunti walivyoahidi kujenga si hoja, sembuse muda wa miezi sita waliosema vitakuwa vimekamilika.Cha msingi ni kuwepo kwa viwanja; ambavyo havipo!

Ukosefu wa viwanja ni moja tu ya ahadi ambazo utawala wa Jubilee umefeli kutimiza.

Isitoshe, hata vilivyopo kwa sasa imechukua karibu mwongo huo mzima wa uongozi wao ili kuvikarabati kwa viwango vya kimataifa.

Kinachosikitisha ni kwamba hata viwango hivyo pia havikutimizwa ipasavyo, jambo ambalo limefanya Kenya kushindwa kuandaa mashindano ya kimataifa ya viwanjani, hususan madimba ya soka, kwa ukosefu wa viwanja.

Viwanja ni moja tu kati ya vifaa vya kimsingi vya michezo ambavyo serikali ya kitaifa haikufanikiwa kujenga.

Wengi wa wanaspoti wetu wamelazimika kujinyima ili kutoa senti mifukoni mwao kununua vifaa, hata wanapjiandaa kwenda kwa mashindano ya kimataifa ambako huiletea taifa sifa kemkem.

Sababu kuu ya serikali kufeli katika sekta ya michezo ni bajeti duni ambayo hutengewa michezo kila mwaka.

Kwa mfano, Sh15 bilioni zilizotengwa mwaka huu haziwezi kujenga viwanja viwili vya kiwango cha kimataifa kuvutia mashindano yoyote yale ya haiba.

Ni katika fedha hizo hizo ambapo pia serikali inatarajia kufadhili shughuli za mashirikisho mbalimbali. Kampeni za siasa zinapozidi kunoga tunataka kusikia hoja za hakika jinsi wawaniaji urais watakavyostawisha michezo nchini.

Pasipo uwekezaji wa kutosha katika miundomsingi ya spoti, tusitarajie wanamichezo wetu kuendelea kung’aa duniani wala vipaji vipya kuchomoza mashinani.

  • Tags

You can share this post!

Madai wizi wa kura yanavyotishia Ruto

Ruto aidhinishwa rasmi na IEBC kuwania urais

T L