• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Madai wizi wa kura yanavyotishia Ruto

Madai wizi wa kura yanavyotishia Ruto

CECIL ODONGO na LEONARD ONYANGO

MADAI ya Naibu Rais William Ruto kuhusu kuwepo kwa njama ya wizi wa kura za urais huenda yakamfanya apotezemaelfu ya wapiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanaonya kuwa, madai hayo yatasababisha wapigakura katika ngome za Naibu wa Rais kukata tamaa na kukataa kujitokeza kupiga kura Agosti 9.

Akiwa katika mkutano na mabalozi wa Muungano wa Ulaya (EU) Alhamisi, Dkt Ruto alidai Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) imeyaondoa majina 800,000 ya wafuasi kutoka ngome zake kwenye sajili ya wapigakura.

Dkt Ruto alisema wataandikia IEBC waraka kuhusu suala hilo akisema, tume hiyo lazima ihakikishe kuwa uchaguzi unaendeshwa kwa haki na njia huru.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati alikashifu matamshi ya Dkt Ruto akisema kuwa sajili ya IEBC haijavurugwa wala hakuna jina la mpiga kura ambalo limeondolewa.

Bw Chebukati mnamo Jumanne alikiri kuwa baadhi ya maafisa wa tume hiyo walihamisha majina ya wapigakura kutoka kituo kimoja hadi kingine bila idhini yao na akaahidi watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Hata hivyo, wadadisi wanasema kauli ya Dkt Ruto huenda ikamponza na inaonyesha kuwa amekosa imani katika utendakazi wa IEBC, tume ambayo alisifu 2017 akisema iliandaa uchaguzi huru waliposhinda hatamu yao ya pili pamoja na Rais Uhuru Kenyatta.

Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Martin Andati, kauli ya Dkt Ruto ni ya kutayarisha wafuasi wake waamini kuwa uchaguzi utaibwa na kuwasababisha wakatae matokeo yake.

“IEBC ina makamishina ambao hawatoki kabila moja na ni vigumu sana waafikiane kuwa majina ya watu wa kabila fulani, yaondolewe katika sajili ya wapigakura. Naibu Rais anawatayarisha wafuasi wake kisaikolojia wakatae matokeo ya uchaguzi,” akasema Bw Andati.

“Kauli hiyo inaweza kumponza hasa eneo la Kati ambako amekuwa na uungwaji mkono tangu 2017. Wakazi huenda wakaamua kutoshiriki uchaguzi wakisema ushaamuliwa na kura zao hazitakuwa na umuhimu wowote ikizingatiwa mara hii pia hawana mwaniaji maarufu ambaye anaweza kutwaa urais kutoka eneo hilo,” akaongeza.

Naye Bw Javas Bigambo, ambaye pia ni mdadisi wa masuala ya siasa anasema kuwa kuwa, japo madai hayo yanaathiri kura za Dkt Ruto, yanasaidia kuhakikisha kuwa IEBC inaandaa uchaguzi huru na wa haki.

“Yamkini Naibu wa Rais Ruto anafahamu kuwa madai ya wizi wa kura yanakatisha tamaa wafuasi wake. Hiyo ndiyo maana analalamika na kisha kukimbia katika mikutano ya kampeni kuwahakikishia kuwa kura zake haziwezi kuibwa,” anasema Bw Bigambo.

Anasema madai hayo ya wizi wa kura yanawapa wapinzani wa muungano wa Azimio silaha ya kumshambulia kwa madai kwamba amehisi kuwa atapoteza uchaguzi.

Kwa mujibu wa wakili Danstan Omari, kauli hiyo huenda ikapunguza idadi ya wale ambao watajitokeza katika ngome ya Dkt Ruto.

Pia Bw Omari anasema kuna uwezekano Dkt Ruto anatumia hiyo kama propaganda ya kuwazindua IEBC kazini ili wahakikishe kuwa wanaendesha majukumu yao kwa uwazi na wasipendelee mrengo wa Bw Odinga unaoungwa mkono na serikali.

“Huu ni ujanja anaoutumia Dkt Ruto ambaye anatumia mbinu zilizotumika na Raila Odinga mnamo 2017,” akasema wakili Omari.

  • Tags

You can share this post!

Watu wanane waangamia kwenye ajali mbaya Narok

TAHARIRI: Utawala wa Jubilee hauna cha kujivunia kuhusu...

T L