• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 10:55 AM
TAHARIRI: Viongozi washirikiane mwaka huu kuwafaa raia

TAHARIRI: Viongozi washirikiane mwaka huu kuwafaa raia

NA MHARIRI

BAADA ya mbwembwe za kusherehekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, lisilofichika ni kwamba wananchi wazalendo wamevuka mwaka wakiwa na matarajio kwamba serikali ya Kenya kwanza itaamka usingizi na kutatua changamoto zinazowakumba na kubadilisha hali yao ya maisha kama ilivyokuwa ahadi yao.

Raia wakiishi katika mazingira na maisha ya matatizo na ugumu wa maisha mara nyingi hugeuka mzigo kwa serikali kiasi cha kushindwa kutawala.

Watu bila kupata elimu bila ugumu, ajiri bila upendeleo, maendeleo kwa usawa na haki mahakamani bila ubaguzi mara nyingi nchi huishia kutishika na kukosa amani , umoja na maendeleo.

Haitakuwa busara kwa Rais Willam Ruto na serikali yake kukosa kutia bidii kuimarisha usalama wa raia mwaka wa 2023, kukuza ushirikiano, utangamano na amani kwa viongozi wote akiwemo Raila Odinga na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta maana Rais ndiye nguzo ya amani (katiba kifungu cha 131(e)), kuanzisha mikakati ya kufanyia ukarabati sera zinazokandamiza umma, kuboresha uchumi na kufufua miradi iliyokwama, hatuna haja na mbinu zake kubomoa Azimio bali tunataka mikakati yake kubomoa umaskini kwa raia.

Huu ndio mwaka ambao viongozi wa kisiasa wanafaa kushirikiana bila kujali ikiwa wako serikalini au upinzani kubadilisha maisha ya raia kwa kutetea maslahi yao badala ya kutumia muda mwingi kugombana kwa manufaa yao kisiasa.

Huu si mwaka wa wanasiasa wa upinzani kujipendekeza na kujiunga upande wa serikali au kuanza kujivumisha kwa ajili ya kampeni za 2027 au kuunda vyama vya kikanda.

Aidha, si kipindi cha wanasiasa wa Kenya kwanza kuanza kutangatanga wakijipiga kifua huku wakisifia utendakazi wa serikali bali wajitolee kusuka mikakati kusaidia bei ya unga kushuka kama alivyoahidi Rais Ruto na kutatua changamoto za ukosefu wa ajira na chakula cha kutosha nchini.

Ni hali ya kutia hofu kujua wanasiasa wetu hupenda zaidi kugombana na kugawanyika katika makundi mawili tu wakati wanaposhughulikia swala linalonuiwa kumfaa mwananchi huku wakishirikiana kama sahani na kijiko wanaposhughulikia mahitaji yao kisiasa.

Hulka hii ni hatari na imekuwa chanzo cha taifa hili kukosa kufanikiwa kujenga msingi dhabiti wa uchumi bora miaka mingi baada ya uhuru wetu na kuwa chanzo cha wakenya kuendelea kusakamwa na matatizo ya kila aina.

Mwaka huu tunatarajia serikali ya kitaifa kushirikiana na serikali za kaunti 47 kufaulisha miradi iliyokwama mashinani na kujenga nyumba kuwafaa raia wanaoishi Katika mitaa ya mabanda huku tukiendelea kupanda miti katika juhudi za kulinda mazingira.

  • Tags

You can share this post!

Vita Chelsea, Man City FA leo Man Utd ikiitandika Everton

Shirikiana ndio, lakini msimezwe na Ruto, Raila aambia...

T L