• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Vita Chelsea, Man City FA leo Man Utd ikiitandika Everton

Vita Chelsea, Man City FA leo Man Utd ikiitandika Everton

NA MASHIRIKA

CHELSEA watatua ugani Etihad leo Jumapili kwa mechi ya raundi ya tatu ya Kombe la FA itakayowapa fursa ya kulipiza kisasi dhidi ya Manchester City waliowapokeza kichapo cha 1-0 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Alhamisi uwanjani Stamford Bridge.

Pambano hilo litakuwa la tatu kukutanisha Man-City na Chelsea katika kipindi cha miezi miwili; na la pili chini ya siku nne. Man-City kwa sasa wanakamata nafasi ya pili katika jedwali la EPL kwa alama 39, tano nyuma ya Arsenal wanaoselelea kileleni baada ya kutandaza pia mechi 17.

Japo kiu ya kocha Pep Guardiola ni kuongoza waajiri wake kuwafikia kisha kuwapiku Arsenal kileleni mwa jedwali la EPL, Mhispania huyo anakamia pia kunyanyua Kombe la FA kwa mara ya pili tangu 2018-19.

Miaka mitatu baada ya kuponda Watford 6-0 katika fainali ya Kombe la FA, Man-City wameaga kipute hicho mara tatu mfululizo kwenye hatua ya nusu-fainali.

Liverpool walitawazwa wafalme wa msimu jana baada ya kufunga Chelsea penalti 6-5 kufuatia sare tasa mwishoni mwa muda wa ziada.

Miamba hao walikomoa Man-City 3-2 katika nusu-fainali baada ya Arsenal na Chelsea kuwadengua katika hatua hiyo mnamo 2020 na 2021 mtawalia.

Ushindi wa tatu mfululizo dhidi ya Chelsea utawapa Man-City motisha zaidi ya kutandika Southampton katika raundi ya nne ya Carabao Cup ugani St Mary’s mnamo Januari 11, siku tatu kabla ya kualika Manchester United kwa gozi kali la EPL uwanjani Etihad.

Nafuu zaidi kwa Man-City ni wingi wa visa vya majeraha katika kambi ya Chelsea itakayokosa maarifa ya zaidi ya wanasoka 10 tegemeo wakiwemo Mason Mount, Raheem Sterling, Christian Pulisic, Reece James, Armando Broja, N’Golo Kante na Edouard Mendy.

Kichapo cha nne kutokana na michuano sita mfululizo ya EPL iliacha Chelsea katika nafasi ya 10 jedwalini kwa alama 25 huku pengo la pointi 10 likitamalaki kati yao na nambari nne Man-United waliocharaza Everton 3-1 katika Kombe la FA mnamo Ijumaa ugani Old Trafford.

Man-United walifungua ukurasa wa mabao kupitia Antony ds Santos katika dakika ya nne kabla ya Conor Coady kusawazishia Everton.

Hata hivyo, Coady alijifunga mwanzoni mwa kipindi cha pili na kuwapa Man-United bao la pili kabla ya Marcus Rashford kufunga penalti sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Huku Man-City wakiaga Kombe la FA katika nusu-fainali mara tatu mfululizo, Chelsea wamepoteza fainali tatu zilizopita za kipute hicho baada ya kulemewa na Arsenal, Leicester City na Liverpool kwa usanjari huo.

Hofu zaidi kwao ni kwamba watatua leo ugani Etihad wakiwa na rekodi duni ya kupoteza mechi nne zilizopita za ugenini katika mashindano yote.

Kabla ya kujizolea alama tatu ugani Stamford Bridge mnamo Alhamisi, Man-City walikuwa wamepepeta Chelsea 2-0 katika raundi ya tatu ya Carabao Cup mnamo Novemba 9.

Hata hivyo, Chelsea wameshinda mechi zote mbili zilizopita dhidi ya masogora wa Guardiola katika Kombe la FA. Aymeric Laporte na Ruben Dias ndio wanasoka wa pekee watakaokosa kuwa sehemu ya kikosi cha Man-City.

Arsenal ambao ni mabingwa mara 14 wa Kombe la FA watamenyana kesho na Oxford United ya Ligi ya Daraja ya Pili (League One) uwanjani Kassam.

Kila kikosi kitakachoshinda mechi ya raundi ya tatu kitatuzwa Sh15 milioni kutoka kwa waandalizi wa Kombe la FA.

  • Tags

You can share this post!

Wafanyakazi Posta hawajalipwa miezi 4

TAHARIRI: Viongozi washirikiane mwaka huu kuwafaa raia

T L