• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 9:55 AM
TAHARIRI: Vitengo vyote vya kukabili ugaidi viwe macho zaidi

TAHARIRI: Vitengo vyote vya kukabili ugaidi viwe macho zaidi

NA MHARIRI

UFICHUZI uliotolewa mahakamani mjini Mombasa kwamba magaidi wa Al-Shabaab wametuma watu saba kutekeleza shambulio nchini, wafaa kushughulikiwa kwa haraka.

Polisi wa Kitengo cha Kupambana na Ugaidi (ATPU) wanapaswa kushirikiana na wenzao wa Kituo cha Kushughulikia magaidi (NCTC), ili kupata maelezo ya kutosha na kuzuia kuzuka kwa shambulizi lolote.

Kuwepo kwa habari za mashambulizi ya kigaidi wakati huu ambapo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inatarajiwa kutangaza muda wa kampeni, si habari nzuri.

Wahuni wanaweza kuwatumia magaidi kutekeleza maslahi yao ya kisiasa, jambo ambalo linaweza kusababisha machafuko.

Vitengo vyote viwili vipo chini ya wizara ya Usalama na Masuala ya Ndani katika Afisi ya Rais. Ina maana kuwa wakurugenzi wa ATPU na NCTC hutoa ripoti zao kwa Baraza la Kitaifa la Usalama.

Ushauri wao safari hii, wafaa kueleza wahusika kwamba, mbali na vitengo hivyo viwili, polisi wa kawaida wanaokaa kwenye maeneo karibu na mipaka yetu wanapaswa kupata mafunzo.

Wizara ya Usalama inapaswa kufanyia mageuzi mfumo wa mafunzo ya polisi, ili kupenda nchi (Uzalendo) liwe somo kuu mbali na kufunzwa kukimbia na mazoezi mengine ya viungo.

Kuingia kwa magaidi mara nyingi huwa kupitia mipaka.

Si mara mbili wala tatu, polisi walio karibu na Nairobi ndio ambao wamekuwa wakiwakamata raia wa Ethiopia wakisafirishwa kwenda Afrika Kusini kati ya mataifa mengine ya nje.

Magaidi kupenya na kufika Nairobi au Mombasa ambako hupanga jinsi ya kuendeleza mashambulio, ni ishara kuwa kuna tatizo katika idara ya polisi na maafisa wa Idara ya Uhamiaji.

Mkenya anapotaka kuingia nchi jirani kama Tanzania, huhangaishwa sana kwenye mipaka ya Namanga, Horohoro au Taveta, iwapo hana pesa. Maafisa hao huhangaisha sana watu wasiokuwa na cha kuwapa. Lakini mtu yeyote aliye tayari kutoa kitu kidogo, huchukuliwa kama mfalme na hata kusindikizwa.

Jambo hili linaonyesha wazi kuwa maafisa wetu wa usalama na uhamiaji mipakani, hawajali usalama wa raia wa Kenya, bali senti kidogo wanazopokea.

Kama si hivyo, inawezekanaje magaidi kupenya nchini kutoka kwao Somalia, na kufika katikati ya jiji la Nairobi bila mtu yeyote kuwaona?

  • Tags

You can share this post!

Al-Shabaab saba kushambulia Kenya – ripoti mahakamani

Raila asukumwa na washirika wake

T L