• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Raila asukumwa na washirika wake

Raila asukumwa na washirika wake

NA JUSTUS OCHIENG

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga amesalimu amri ya washirika wake katika muungano wa Azimio kuhusu wito kwa wafuasi wake kuwa wachague wawaniaji wa ODM pekee kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Hii imewadia siku moja tu baada ya mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta katika Azimio kushinikiza mwaniaji wa ODM, Tim Wanyonyi, ampishe Polycarp Igathe kuwa mgombeaji wa ugavana wa Nairobi katika mrengo huo.

Hii ni licha ya mbunge huyo wa Westlands kuwa kwenye kampeni kwa miezi kadhaa na pia kuwa na uzoefu wa siasa.

Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe, alikuwa amemuonya Bw Odinga dhidi ya kuwataka wafuasi wake kuchagua wawaniaji wenye tiketi ya ODM pekee, akisema huenda hatua hiyo ikahujumu Azimio.

Bw Murathe na viongozi wengine walisema kwamba itakuwa njia nzuri kuruhusu ushindani kuwepo baina ya vyama vilivyobuni mrengo huo, wakiwemo wawaniaji huru.

Walisema ni hatua ambayo itachangia wapigakura wengi zaidi kujitokeza ili kushiriki kwenye zoezi hilo.

“Uwepo wa wawaniaji wengi utachangia wapigakura zaidi kujitokeza kushiriki kwenye zoezi hilo. Kwa mfano, ukimjumuisha mwaniaji kutoka chama cha UDM chake David Ochieng, ambacho ndicho anatumia Bw Nicholas Gumbo kuwania ugavana katika Kaunti ya Siaya, itakuwa hatua nzuri. Hili ni ikizingatiwa kuwa wapigakura hao watampigia kura Bw Odinga. Ni mwelekeo mzuri kwani vyama hivyo vyote vitawarai wafuasi wao kujitokeza kumpigia kura Raila kuwa rais,” akasema Bw Murathe kwenye mahojiano naTaifa Leo.’

Akiwahutubia washirikishi wa muungano huo kutoka kaunti 44 jijini Nairobi jana Jumatano, Bw Odinga aliondoa wasiwasi ambao umeibuka kutokana na wito wake.

“Mimi ni mwaniaji urais wa muungano wa Azimio. Wakati ninafanya kampeni zangu katika sehemu tofauti nchini, ninajiuza kama mwaniaji urais wa Azimio. Sitaonyesha mapendeleo yoyote kwa wawaniaji wa ODM bali nitawachukuliwa kwa njia sawa,” akasema Bw Odinga alipohutubu katika Wakfu wa Jaramogi Oginga Odinga (JOO).

Aliandamana na Afisa Mkuu Mtendaji wa muungano huo, Bw Raphael Tuju, wanachama wa bodi ya kampeni yake ambao ni magavana Ndiritu Muriithi (mwenyekiti), Charity Ngilu (Kitui), James Ongwae (Kisii), Sabina Chege (Mbunge wa Murang’a), Dkt Caroline Karugu (Naibu Gavana, Nyeri) na Bi Fatuma Gedi (Mbunge wa Wajir).

Bw Odinga alisema kuwa anaelewa kuna maeneo ambako wapigakura wengi zaidi watajitokeza ikiwa muungano huo utawasimamisha wawaniaji wengi. Alisema kuwa kila mwaniaji atapewa nafasi sawa.

“Kuna maeneo ambako wapigakura wengi watajitokeza ikiwa tutakuwa na wawaniaji wengi, hivyo kutufaa pakubwa kwenye kinyang’anyiro cha urais. Hata hivyo, kuna maeneo ambako hali itakuwa kinyume. Katika maeneo kama hayo, tutabuni maelewano baina ya wawaniaji wetu ili kuepuka migawanyiko,” akasema Bw Odinga.

Katika Kaunti ya Nairobi, kwa mfano, alipendekeza maelewano baina ya wawaniaji ili kuepuka hali ambapo muungano huo utagawanya kura zake.

“Tunaweza kusema kuwa katika baadhi ya maeneo, turuhusu chama kuwasimamisha wawaniaji huku vyama vingine vikijitoa katika maeneo mengine. Vivyo hivyo, tutaviruhusu vyama vyote kuwasimamisha wagombea wao katika baadhi ya sehemu,” akaongeza.

Alisema kuwa mkakati huo utausaidia muungano huo kuibuka mshindi kwenye nyadhifa za kisiasa na kura ya urais.

Alisema muungano huo utatumia taratibu na taasisi zilizowekwa na vyama vya ODM na Jubilee kuendesha kampeni za urais.

“Kwa mfano, ODM ina taasisi thabiti za kisiasa kutoka vituo vya kupigia kura hadi katika kiwango cha kitaifa. Taasisi hizo zinafaa kuunganishwa ili kuipa nguvu kampeni ya urais,” akaeleza.

Alisema kwamba ikizingatiwa uchaguzi huu unahusu mabadiliko ya serikali moja hadi nyingine, una umuhimu mkubwa kwa Wakenya kama ilivyokuwa kwenye chaguzi za 2002 na 2013.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Vitengo vyote vya kukabili ugaidi viwe macho zaidi

Uchunguzi wa mauaji ya Damaris waanza

T L