• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
TAHARIRI: Vituko vya Nick, serikali vyatamausha Starlets zaidi

TAHARIRI: Vituko vya Nick, serikali vyatamausha Starlets zaidi

NA MHARIRI

UFUFUZI wa karakasi kati ya serikali na aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka nchini (KFK), Nick Mwendwa unaamsha machungu tele wanayopitia kinadada wa timu ya taifa ambao ndoto yao ya kushiriki mashindano ya Bara (AWCON) yanayoendelea nchini Morocco, iliyokatizwa ghafla.

Mnamo Jumatano, Mahakama ya Kuamua Kesi za Ufisadi ilimwachilia huru Bw Mwendwa kwa kukosa ushahidi wa kesi ambapo anadaiwa kupora Sh38 milioni.

Uamuzi huo ulifkiwa baada ya Mkrugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kukosa ushahidi wa madai hayo ya ulaghai.

Hatua hiyo ilielekea kuleta tumaini la kutamatika kwa vita kati ya FKF na serikali vilivyoshuhudiwa Novemba 2021.

Tukio hili lilitokea wiki moja tu baada ya matawi ya FKF nchini kutangaza mwelekeo kuhusu mechi za KPL msimu ujao. Wapenzi wa soka nchini walikuwa wameanza kuona mwangazi baada ya kiza cha siku nyingi kilichogubika spoti hii. Kwa wengi, dalili za mwanzo mpya zilikuwa zinabisha kuhusu usimamizi wa soka Kenya.

Sasa huenda ikawa matumaini hayo yalikuwa ndoto ya mchana tu. Siku iliyofuata ya Alhamisi, Bw Mwendwa alitakiwa kufika katika Mahakama ya Kiambu Julai 11, kujibu mashtaka mapya. Afisi ya DPP ilisema ina mashtaka mapya ambayo ilinuia kuwasilisha kortini.

Hali hii ya kutamausha mashabiki wa kandanda inauma zaidi, taswira ya warembo wa kikosi cha taifa wakijikunyatia humu nchini kwa kukosa kuenda Morocco.

Kama hakungekuwa na mivutano kama hii iliyosababisha wao kufungiwa nje, kinadada hawa wa nyumbani wangekuwa wakituwakilisha huko ugenini.

Wiki hii, kocha wa zamani wa Harambee Starlets alielezea imani yake kwa kikosi cha Starlets kuwa huu ungekuwa mwaka mzuri kwao kutamba kimataifa kama marufuku ya Fifa hayangekuwepo.

Alisisitiza kwamba alikuwa amewanoa vilivyo na kujaa imani wangefuzu ikiwa wangepewa nafasi kucheza na timu ya Crested Crowns ya Uganda.

Mkufunzi huyo alionekana kulaumu wahusika waliochangia mechi hiyo kuondolewa licha ya kinadada hao wazalendo kuwa kambini wakjiandaa kukutana na Waganda hao uwanjani.

Bila shaka mabinti hawa wa Starlets wanapitia machungu, masikitiko na hali ya kufa moyo zaidi wanaposhuhudia mikwaruzano mipya kuhusiana na spoti yao.

Itafaa zaidi ikiwa tatizo hili kuhusu soka litasuluhishwa kabisa ili vijana wetu wapate utulivu wa moyo ili kujivunia ustawi wa talanta na hatimaye kujipatia riziki kwa bidii hizo zao.

You can share this post!

DOMO: Msikizeni shangazi, ana neno!

Kimathi atua Ulaya kutafuta pointi Rally Estonia

T L