• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:55 PM
TAHARIRI: Wadau waungane kumaliza athari za malaria nchini

TAHARIRI: Wadau waungane kumaliza athari za malaria nchini

NA MHARIRI

KENYA leo itajiunga na dunia nzima kuadhimisha Siku ya Malaria Duniani.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Kushinikiza uvumbuzi ili kupunguza athari za malaria na kuokoa maisha.”

Hii ni siku muhimu kwa Kenya, ikizingatiwa kuwa ugonjwa wa malaria ni miongoni mwa maradhi ambayo yamechangia vifo vya mamilioni ya Wakenya tangu miaka ya themanini.

Lakini licha ya athari zake, Kenya imepiga hatua kubwa kukabili maradhi hayo.Miongoni mwa mafanikio ambayo Kenya imepata ni kuzinduliwa kwa chanjo ya kudhibiti maambukizi yake.

Chanjo hiyo ilizinduliwa nchini mnamo 2019, hali iliyoiwezesha Kenya kujiunga na mataifa kama Ghana na Malawi, ambayo yalikuwa yashaanza kutoa chanjo hiyo kwa raia wake.

Tangu uzinduzi huo, Kenya ilianza safari ya kumaliza maradhi hayo nchini kabisa kufikia mwaka 2023.Licha ya juhudi hizo, ni kaunti nne pekee kati ya kaunti 47 nchini ambazo zimeonyesha dalili ya kumaliza maradhi hayo.

Kulingana na Wizara ya Afya, kaunti hizo ni Nyeri, Nyandarua, Kirinyaga na Laikipia.Mwelekeo huu si wa kutia moyo, ikizingatiwa kuwa juhudi nyingi za kukabili maradhi hayo zimekuwa zikiendeshwa sawa katika karibu kila kaunti.

Inasikitisha kuwa licha ya mabilioni ya fedha kutengewa mipango hiyo, huenda Kenya ikakosa kutimiza malengo hayo mwaka ujao.

Moja ya matatizo ambayo yamekuwa yakikumba juhudi hizo ni uporaji wa fedha zinazotengwa na serikali na mashirika ya nje kwa wadau mbalimbali kuendesha mikakati ya kukabili maradhi hayo.

Hili ni tatizo ambalo limeshuhudiwa kwenye mikakati ya kukabili maradhi mengine kama vile virusi vya HIV, virusi vya corona kati ya mengine.

Uporaji wa fedha za kuendesha juhudi hizo ndio umechangia pakubwa Kenya kushindwa kuyamaliza maradhi hayo, ikilinganishwa na nchi nyingine duniani.

Serikali za kaunti ndizo zimekuwa zikilaumiwa pakubwa, kwani imekuwa kawaida kwa idara za afya katika serikali hizo kushirikishwa kwenye mikakati ya kuikabili.

Kwa mfano, magavana katika kauti za maeneo ya Nyanza na Magharibi kama Kakamega, Homa Bay, Siaya na Kisumu, hawajakuwa wakijitokeza kikamilifu kuungana na Serikali ya Kitaifa na wadau wengine kuyakabili maradhi hayo.

Ikumbukwe kuwa, kaunti hizo ndizo huathiriwa sana na maradhi hayo nchini.

Katika hali hiyo, wito mkuu kwa magavana kote nchini ni kufahamu kuwa, wao ndio daraja kuu litakalohakikisha waathiriwa wa malaria wamefikiwa na Serikali na wadau wengine kama Shirika la Afya Duniani (WHO).

Uwajibikaji wao ndio utakaohakikisha Kenya imetimiza lengo la kuyamaliza maradhi hayo kabisa kufikia mwishoni mwa mwaka ujao.

Ujumbe uo huo ndio unaopaswa kukumbatiwa na kila mhusika, kwani ushindi kamili utapatikana tu ikiwa kila mmoja atatia bidii kutekeleza kikamilifu wajibu anaohitajika.

You can share this post!

Rais Kenyatta aongoza Wakenya kuanza kuutazama mwili wa...

Kibarua kipya kwa wazazi wanafunzi wakirejea shuleni

T L