• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 3:08 PM
Kibarua kipya kwa wazazi wanafunzi wakirejea shuleni

Kibarua kipya kwa wazazi wanafunzi wakirejea shuleni

NA WANDERI KAMAU

HUKU wanafunzi waliofanya mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) wakiendelea kusherehekea matokeo yao, wazazi wanakabiliwa na kibarua kipya kuwarejesha wanafunzi shuleni leo Jumatatu.

Shule za msingi kote nchini zimefunguliwa leo, nao wanafunzi waliomaliza Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) wakitarajiwa kujiunga na Kidato cha Kwanza kuanzia Mei 2.

Hapo jana Jumapili, wazazi katika sehemu mbalimbali nchini walikuwa kwenye harakati za mwisho mwisho kuwatayarisha wanao kufungua shule.

Mamia ya wazazi walifurika kwenye maduka ya kuuzia vitabu na sare za shule kuwanunulia vitabu na sare mpya.

Jijini Nairobi, baadhi ya maduka ya kuuzia vitabu yalilazimika kufunguliwa jana kutokana na idadi kubwa ya wazazi waliofika.

Kwa kawaida, maduka mengi huwa hayafunguliwi siku za Jumapili.

Kulingana na Bi Faith Mwangi, ambaye ni muuzaji vitabu katika Duka la Vitabu la Savannis, jijini Nairobi, iliwalazimu kufungua kutokana na idadi kubwa ya wateja.

“Kwa kawaida, huwa tunafungua duka letu kati ya Jumatatu na Jumamosi mchana. Jumapili huwa siku ya kupumzika. Hata hivyo, ikizingatiwa wanafunzi wengi wanafungua kesho, ilitulazimu kuendesha shughuli zetu kama kawaida,” akasema Bi Mungai, kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo.’

Duka la vitabu la Textbook Centre pia lilifunguliwa Jumapili kinyume na kawaida, ili kuwaruhusu wazazi kuwanunulia vitabu vyao.

Kwenye maduka ya kuuzia sare, wazazi walionekana wenye shughuli nyingi kuwapimishia au kuwanunulia wana wao sare mpya.

Hata hivyo, wengi walilalamika kuhusu gharama ya juu ya sare hizo.

Kwenye duka la kuuzia sare la Unique Fashions, lililo kwenye Barabara ya Muindi Mbingu, wazazi walilazimika kupanga foleni ili kungoja kuhudumiwa.

Wengi walisema walilazimika kufanya hivyo kwani maduka mengi hayakuwa yamefunguliwa au yanauza sare kwa bei za juu.

“Si kupenda kwetu kupanga foleni. Bei za hapa ni za chini ikilinganishwa na maduka mengine,” akasema Bw Francis Omondi, aliyeandamana na mwanawe, aliye katika Darasa la Saba.

Kwenye steji za matatu, kulikuwa na misongamano mikubwa ya watu, baadhi ya wazazi wakiwarejesha wanao wanaosomea katika maeneo ya mbali.Baadhi ya mashirika ya matatu pia yaliongeza nauli, yakitaja bei ya juu ya mafuta kama chanzo cha kuchukua hatua hiyo.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Wadau waungane kumaliza athari za malaria nchini

Kundi lapendekeza Ruto ateue Waiguru kuwa naibu wake

T L