• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
VALENTINE OBARA: Kuna kila ishara uchaguzi mkuu ujao huenda ukaibua mtafaruku

VALENTINE OBARA: Kuna kila ishara uchaguzi mkuu ujao huenda ukaibua mtafaruku

NA VALENTINE OBARA

MATUKIO mawili ambayo yameshuhudiwa kaunti tofauti za Pwani hivi majuzi, yanaibua wasiwasi kuhusu hali itakavyokuwa kampeni za kisiasa zitakapoanza rasmi na hatimaye Uchaguzi Mkuu kuandaliwa Agosti.

Takribani wiki mbili zilizopita, fujo zilizuka katika mkutano wa wajumbe wa chama cha ODM uliofanywa Kilifi.

Fujo hizo zilikuwa kati ya wafuasi wa wanasiasa wanaomezea mate tikiti ya chama hicho kuwania viti vya kisiasa katika uchaguzi ujao.

Wikendi iliyopita, hali sawa na hiyo ikashuhudiwa tena katika Kaunti ya Mombasa wakati wa mkutano wa hadhara ambao uliongozwa na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga.

Katika mkutano huo uliofanywa uwanjani Tononoka, vijana wanaoaminika kuwa wafuasi wa wanasiasa ambao wanataka tikiti ya ODM kurithi kiti cha Gavana Hassan Joho, walirushiana makonde na hata wakati mmoja kumrushia kifaa Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, alipokuwa akihutubu jukwaani.

Baadhi ya wanasiasa, akiwemo Bw Odinga na Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw Edwin Sifuna, walikemea wazi matukio hayo lakini hilo halikukomesha fujo kuendelea katika uwanja huo.

Kinachosikitisha ni kuwa, wasimamizi wa kampeni za baadhi ya wanasiasa walisherehekea visa hivyo.

Swali tunalofaa kujiuliza ni, kama tumeanza kushuhudia visa aina hii ndani ya vyama wakati huu ambapo hata kura za mchujo hazijafanywa, hali itakuwaje wakati wa mchujo, wakati wa kampeni za chama kimoja dhidi ya kingine, na hata wakati uchaguzi utakapowadia na mshindi kutangazwa?

Siasa ni jambo ambalo huibua hisia kali miongoni mwa wananchi wengi kwa kiwango cha kupumbazwa kirahisi ili waingie vitani dhidi ya majirani wao walio na misimamo tofauti.

Ni aibu tunaposhuhudia baadhi ya wanasiasa na vikosi vyao wakifurahia fujo za aina yoyote ile wakati juhudi nyingi zinawekwa na wengine ili kuzuia uhasama unaoweza kuzamisha taifa hili.

Pwani ni mojawapo ya maeneo ya kipekee nchini ambapo kuna watu wa dini, makabila na matabaka tofauti.

Hii inafanya eneo hili kuwa na uwezekano wa kulipuka ghasia za kisiasa kirahisi kwani wanasiasa wachochezi wanaopenda fujo hutumia sana masuala haya kusababisha mgawanyiko katika jamii kwa manufaa yao ya kibinafsi.

Katika chaguzi kuu za miaka iliyopita, eneo hilo halikuepuka kuathirika kwa ghasia za kisiasa na dalili zinazoonekana hivi sasa zinaonyesha huenda tukatumbukia katika hali hiyo tena mwaka huu ikiwa hatutakuwa waangalifu.

Tukumbuke kwamba tukikubali kuingizwa kwa fujo zitakazoathiri uchumi zaidi, wanasiasa wanaotuchochea watakuwa wanaendelea na maisha yao ya kifahari huku raia wa kawaida akikosa hata jirani wa kumwomba maji ya kunywa.

  • Tags

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Eunice David

TAHARIRI: Si lazima lugha ya mama iwe ya kugawanya raia wa...

T L