• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 7:52 PM
VALENTINE OBARA: Ni fedheha kuu wanasiasa kushindana na magaidi

VALENTINE OBARA: Ni fedheha kuu wanasiasa kushindana na magaidi

NA VALENTINE OBARA

WAZEE wa busara walisema, mgeni njoo mwenyeji apone.

Lakini katika msimu huu wa kisiasa, baadhi ya wanasiasa wanaoendelea kuzuru Pwani wanaibua tishio la kutatiza amani ambayo imedumu kwa muda mrefu.

Katika siku za hivi majuzi, wawaniaji urais wamekuwa wakiandamana na vikosi vyao vya wanasiasa kutoka pembe tofauti za nchi kujitafutia kura Pwani.

Ni matarajio ya wengi kuwa, mwanasiasa yeyote, awe anatoka upande wowote ule wa nchi au Pwani, anatambua masuala tatanishi ya kila sehemu ya nchi.

Jinsi ambavyo sheria imetoa nafasi kwa raia yeyote kujiandikisha kuwania wadhifa wa kisiasa katika sehemu yoyote ya nchi ndivyo vivyo hivyo ingetarajiwa wanasiasa wajue wanapotembelea sehemu fulani, kuna mambo wanayofaa kujiepusha nayo.

Ninarejelea haya kwa kuwa nilishtuka sana hivi majuzi kutokana na matamshi ya Gavana wa Machakos, Dkt Alfred Mutua.

Dkt Mutua ambaye ni kiongozi wa chama cha Maendeleo Chap Chap, alikuwa ameandamana na Naibu Rais William Ruto kwa msururu wa kampeni katika kaunti tofauti za Pwani.

Alipokuwa katika mojawapo ya mikutano ya muungano wa Kenya Kwanza mjini Mombasa, gavana huyo alitoa matamshi ya kutisha kuhusu masuala ya kidini.

Katika hotuba yake, Dkt Mutua alipokuwa akiwakanya wakazi dhidi ya kupigia kura chama cha Azimio la Umoja-One Kenya, alidai kuwa mgombea mwenza wa urais katika chama hicho, Bi Martha Karua, ni qafir kwa hivyo hastahili kuchaguliwa mamlakani.

Ijapokuwa katika lugha neno hilo huenda likaonekana kuwa la kawaida, kumaanisha mtu asiyeamini dini yoyote, hilo ni neno ambalo limehusishwa na uchochezi wa kidini katika miaka iliyopita.

Mwanasiasa wa hadhi ya Dkt Mutua ambaye amewahi kuwa msemaji wa serikali ya kitaifa na hata kuonyesha azma ya kutaka kuwania urais, hafai kamwe kupuuza hatari ya kuchochea umma dhidi ya viongozi wenzake kwa msingi wa kidini.

Katika ukanda wa Pwani, masuala ya kidini huwa ni mazito. Hii ni kutokana na kuwa, makundi ya kigaidi yanayojificha nyuma ya dini kutekeleza ukatili dhidi ya raia wasiokuwa na hatia hutumia uchochezi aina hiyo kufanya maovu yao. Baadhi ya viongozi wa kisiasa na maafisa wa mashirika mbalimbali ya umma walijitolea mhanga katika miaka iliyopita kuzima tofauti za kidini zilizokuwa zikitumiwa na magaidi kuhangaisha eneo la Pwani.

Ukanda huu unazidi kupitia athari mbaya za mashambulio ya kigaidi ya miaka iliyopita hadi leo kwani utalii bado haujarudi kwa kiwango kilichokuwepo kabla visa vya ugaidi vilipoanza kutokea.

Kuelekea kwa uchaguzi ujao, wananchi wangependa zaidi kusikia mipango ya viongozi kuhusi jinsi matatizo yanayowakumba yatakavyotatuliwa.

Raia wamepitia hali ngumu mno kwa muda mrefu katika kipindi cha pili cha utawala huu, hasa kutokana na matatizo yaliyosababishwa na kuongezwa kwa ushuru wa bidhaa muhimu za nyumbani na janga la virusi vya corona lililotikisa ulimwengu mzima.

Ni aibu kwa kiongozi kusimama jukwaani kutoa matamshi ambayo yanaweza kudhuru zaidi hali ya maisha ya mwananchi anayemtarajia kutoa suluhu ya jinsi atampunguzia mzigo wa kimaisha.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Uteuzi: IEBC ifuate ushauri wa EACC kuhusu...

Monkeypox imeathiri 1,400 Afrika – WHO

T L