• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
TAHARIRI: Uteuzi: IEBC ifuate ushauri wa EACC kuhusu wanasiasa watiliwao shaka

TAHARIRI: Uteuzi: IEBC ifuate ushauri wa EACC kuhusu wanasiasa watiliwao shaka

NA MHARIRI

WIKI chache zilizopita, Tum e Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilinukuliwa ikisema itaamua hatima ya Kinara wa Wiper kalonzo Musyoka, kutokana na matakwa ya umma.

Wakati huo, IEBC ilisema itamjumuisha Bw Musyoka kwenye orodha ya watakaowasilisha nyaraka za kutaka urais. Iwapo hakutatokea yeyote kupinga jambo hilo, basi ataidhinishwa kuwa miongoni mwa watakaokuwa debeni Agosti 9.

Bw Musyoka amealikwa kuwasilisha stakabadhi zake Jumamosi katika ukumbi wa Bomas of Kenya, kuwania urais kupitia chama chake cha Wiper. Amechukua hatua hiyo huku nyaraka zilizo na Msajili wa Vyama vya Kisiasa Bi Anne Nderitu, zikionyesha kuwa chama cha Wiper ni mojawapo ya vyama vinavyounda muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Alliance.

Kama IEBC iko tayari kumzuia Bw Musyoka iwapo kutatokea pingamizi, basi sasa tume hiyo ina kibarua cha kuangalia upya maamuzi yake ya wiki hii.

Jana, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), ilitoa orodha ya watu wanaosemekana kutiliwa shaka katika mienendo yao. EACC iliorodhesha majina ya wanasiasa zaidi ya 300 iliyosema wanastahili kupigwa msasa na ikiwezekana wanyimwe fursa ya kushiriki kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.

Ingawa baadhi yao wanashukiwa kuwa hawakuwa wamejiuzulu kutoka kwa serikali kufikia Februari 9, idadi kubwa ni ya wale walioshtakiwa kuhusiana na madai ya ufisadi.

Kwa mujibu wa Sura ya Sita ya Katiba, watu wanaotiliwa shaka kuhusu maadili na ufisadi hawafai kuruhusiwa kutafuta nafasi za uongozi. Kifungu cha 75 cha Katiba kinaweka wazi sifa za ntu anayefaa kuwa Afisa wa Serikali. Mambo ambayo baadhi ya wanaotaka nyadhifa wanashukiwa kutekeleza, yanakiuka kabisa kifungu hicho.

Iwapo mtu alifikishwa mahakamani na kushtakiwa kuwa alihusika na wizi wa pesa za umma, au hata akafungwa jela kwa makosa hayo, ni makosa kwa IEBC kumuidhinisha. Jukumu la kufasiri iwapo mahakama itamruhusu au la ni la idara ya Mahakama wala si IEBC.

Miaka 12 tangu tuipitishe Katiba, tume ya uchaguzi inapaswa kuwa inayoweza kuonyesha mfano wa jinsi sheria inavyotekelezwa bila mapendeleo.

Matatizo ya nchi yoyote hutokana na jinsi inavyochagua viongozi wake. Kama alivyowahi kusema hayati Rais Daniel arap Moi, siasa mbaya husababisha maisha mabaya. Kama mwanasiasa amehusishwa na wizi wa pesa za umma, kumruhusu awanie uongozi ni kama kuidhinisha tabia yake.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati atambue kuwa anaungwa mkono na wananchi. Asiogope kufanya maamuzi magumu.

You can share this post!

Rais Bio asimulia jinsi Kenya ilivyosaidia Sierra Leone

VALENTINE OBARA: Ni fedheha kuu wanasiasa kushindana na...

T L