• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
VALENTINE OBARA: Watu kupotezwa: Serikali ithibitishe kuwa haihusiki

VALENTINE OBARA: Watu kupotezwa: Serikali ithibitishe kuwa haihusiki

Na VALENTINE OBARA

MALALAMISHI yanayoongezeka kutoka kwa mashirika ya kutetea haki za kijamii, baadhi ya viongozi na wananchi kuhusu watu ‘kupotezwa’ huharibia taifa hili sifa kuhusu kujitolea kwake kuheshimu haki za kibinadamu.

Kila mwaka, visa hivyo ambavyo vingi hutokea maeneo ya Pwani huwa havikosekani.

Idara ya polisi hulaumiwa kwa madai ya kuhusika katika utekaji nyara wa watu ambao wengi wao hutokomea bila kujulikana waliko huku wengine wakipatikana wamefariki.

Licha ya wakuu wa polisi kukana kuhusika, maswali huibuka kuhusu kwa nini hawawezi kutumia mamlaka yao kuwatafuta watu ambao huripotiwa kuwa wametoweka kwa njia zisizoeleweka.

Ikizingatiwa kuwa idadi kubwa ya wanaotoweka kwa njia hizi huwa ni washukiwa wa ugaidi au aina nyingine za uhalifu, wananchi wengi huwa hawana budi ila kujijazia wenyewe kuwa idara ya polisi ndiyo mshukiwa mkuu.

Kulingana na ripoti ya shirika la Haki Africa, jumla ya watu 61 walipotezwa katika hali isiyoeleweka nchini mwaka huu ambapo 30 kati yao ndio waliopatikana wakiwa hai ilhali wengine wanane wakapatikana wakiwa wamefariki.

Eneo la Pwani ndilo liliongoza kwa idadi kubwa ya watu ambao walitoweka jinsi hiyo, kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Haya ni matukio ambayo si changamoto kwa Kenya pekee kwani ni mambo ambayo hushuhudiwa pia katika nchi nyingine kimataifa.

Mashirika ya kimataifa yanayotetea haki za binadamu huashiria kuwa mara nyingi polisi hushukiwa kuhusika kwa vile asasi za serikali zinazopambana na uhalifu hutaka njia za mkato za kutoa hukumu bila kupitia mahakamani.

Kile kinachojitokeza ni kuwa wakati mwingi aina ya uhalifu ambao waathiriwa huhusishwa nao hufanana, kuanzia kwa ugaidi, ulanguzi wa mihadarati au aina nyingine ya uhalifu sugu.

Hata hivyo, kuna madai kuwa wakati mwingine magenge ya uhalifu hutekana nyara wenyewe kwa wenyewe wakati mizozo inapotokea baina yao.

Madai haya huenda yakawa na uzito kwa kiwango fulani hasa machoni mwa wale wanaotaka kuondolea serikali lawama kuhusu visa hivi.

Hata hivyo, zigo la kujiondolea lawama limo mikononi mwa serikali na hilo litawezekana tu kukiwa na thibitisho kamili kwamba polisi kamwe hawahusiki.

Isisahaulike kuwa baadhi ya wakuu wa usalama nchini huwa wamekiri kuna maafisa ambao wamepotoka kimaadili na huenda huwa wanatumiwa kutekeleza utekaji nyara au hata mauaji ya washukiwa, ila sababu za wao kutumiwa kwa njia hizo haziko wazi.

Kivyovyote vile, kilicho muhimu ni serikali kusafisha jina lake hasa idara ya polisi kuhusu visa hivi.

Njia pekee ya kuthibitisha kuwa serikali haihusiki ni kwa kutuonyesha ni nani anayehusika.

Ilivyo kwa sasa, maelezo mengi yanayotolewa huashiria mkono wa polisi ulihusika.

Visa hivi vinaporipotiwa kwa polisi, vichukuliwe sawa na vya wananchi wengine wanaopotea ili kama kweli polisi hawahusiki, magenge yanayodaiwa kuhusika yasakwe na kuzimwa kwani ni wazi yanaweza kuwa hatari kwa usalama wa raia wengine wote.

  • Tags

You can share this post!

Wanariadha waalikwa kushiriki Mbio za Nyika za Mombasa

KINYUA BIN KING’ORI: NCIC ikomeshe wanasiasa ambao...

T L