• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
WANDERI KAMAU: Kibaki ndiye ‘Musa’ aliyekomboa nchi kutoka kwa uongozi dhalimu

WANDERI KAMAU: Kibaki ndiye ‘Musa’ aliyekomboa nchi kutoka kwa uongozi dhalimu

NA WANDERI KAMAU

INGAWA kifo ndicho hatua ya mwisho ya maisha ya kila mwanadamu hapa duniani, baadhi ya vifo huwa vichungu sana.

Huwa vigumu kukubali na kuamini kwamba, baadhi ya watu tuliowaenzi na kuwapenda wametuacha.

Kwa mantiki hiyo, moja ya matukio hayo machungu ni kifo cha Rais Mstaafu Mwai Kibaki, aliyefariki Ijumaa.

Kwa kizazi kilichozaliwa kuanzia 2000, huenda ikawa vigumu kidogo kwao kufahamu mchango mkubwa aliotoa Mzee Kibaki kuistawisha Kenya katika karibu kila nyanja.

Alipotwaa uongozi kutoka kwa marehemu Daniel Moi 2003, nilikuwa katika Darasa la Nane.Nilikuwa miongoni mwa kundi la kwanza la wanafunzi kufaidika kutokana na Mpango wa Elimu Bila Malipo (FPE) alioanzisha Mzee Kibaki baada ya kuchukua uongozi.

Mara tu baada ya ushindi wa Mzee Kibaki, ilikuwa rahisi kuhisi kiwango kikubwa cha matumaini ambacho wanakijiji wengi walikuwa nacho.

Kijijini mwetu, wazee walikongamana kwenye viwanja vya kuwalishia mifugo kujadili jinsi Mungu alikuwa “amewatendea muujiza” kuuwezesha muungano wa Narc kuung’oa mamlakani utawala wa Kanu.

Walirejelea madhila waliyopitia chini ya utawala huo na mapambazuko mapya aliyoleta Mzee Kibaki.

Mashambani, akina mama walisikika wakiimba nyimbo za kuukashifu utawala wa Moi na kumsifu Mzee Kibaki kama “Musa” aliyetumwa na Mungu kuwakomboa Wakenya kutoka kwa utawala wa dhalimu wa Firauni.

Shuleni, wanafunzi wengi walionyesha furaha nyusoni mwao, kwani badala yao kufukuzwa kuendea karo majumbani mwao (kwani huo ndio ulikuwa mtindo kila mwanzo wa muhula), idadi yao iliongezeka maradufu.

Katika vyombo vya habari, ulikuwa mwanzo mpya, kwa kuwa Wakenya walipata nafasi kuanza kusikiliza matangazo kutoka kwa vituo vya redio vya masafa mafupi (FM)—kinyume na ilivyokuwa awali, ambapo ni shirika la habari la KBC pekee lililokuwa likipeperusha matangazo.

Ulikuwa ukurasa mpya kwa kila mmoja!

Tunapojitayarisha kumuaga Mzee Kibaki, ni wazi kuwa yeye ndiye aliyekuwa ‘Musa’ aliyewavusha Wakenya kutoka Misri (utawala wa Kanu) kupitia Bahari ya Shamu hadi nchi ya ahadi ya Kanani.

Mabadiliko mengi tunayoshuhudia katika karibu kila sekta muhimu nchini yanatokana na juhudi alizoweka Mzee Kibaki kuibadilisha Kenya.

Utakapofika mbinguni, Mzee Kibaki, tafadhali wasalimie viongozi wenzako mashuhuri kama Nelson Mandela, Julius Nyerere, Thomas Sankara, Amilcal Cabral kati ya wengine.

Laleni pema, Mzee. Tutaonana baadaye!

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Kibaki asifiwa kama aliyeenzi bidii ya maafisa

Uhuru akwepa kumsalimia Dkt Ruto kwa mkono bungeni

T L