• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
WANTO WARUI: Waziri Machogu ana kibarua kigumu cha kudumisha hadhi ya masomo nchini

WANTO WARUI: Waziri Machogu ana kibarua kigumu cha kudumisha hadhi ya masomo nchini

NA WANTO WARUI

KIFO cha ghafla cha aliyekuwa waziri wa Elimu Prof George Magoha kimelipokonya taifa hili mfanyakazi aliyejitolea hadi akainua hadhi ya masomo nchini.

Katika awamu yake kama waziri wa Elimu, marehemu Magoha, hakuinua tu viwango vya elimu nchini, bali pia alipigania haki za watoto kuwa shuleni hasa kwa kusisitiza kuwa wanafunzi wote waliomaliza shule za msingi, ni sharti wajiunge na shule za sekondari.

Zaidi ya hayo, marehemu Magoha alijitahidi sana kuona kuwa mtaala mpya wa elimu wa CBC umefaulu.

Alifanya kazi nyingi ya kuendeleza masomo ya CBC ambayo mtangulizi wake waziri Amina Mohammed alikuwa amesema kuwa nchi haikuwa tayari kwa masomo hayo. Prof Magoha alikuwa amejenga madarasa ambayo yangetumika na wanafunzi wa CBC iwapo wangejiunga na shule za sekondari.

La muhimu zaidi lililoweza kutekelezwa na marehemu Magoha, ni kuangamiza wizi wa mitihani hapa nchini. Yeye na Waziri Matiang’i watakumbukwa daima kwa kurejesha hadhi ya elimu nchini kwa kukomesha wizi wa mitihani.

Taifa lilikuwa na imani sana na matokeo ya mitihani kutokana na usimamizi na ulinzi bora wa mitihani ilipokuwa ikifanywa hadi kutangazwa kwake.

Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne, KCSE ya 2022 ambayo yangali yanasherehekewa na baadhi ya watu hasa familia zilizotoa wanafunzi waliofuzu vizuri , yameibua maswali kadhaa kutoka kwa wadadisi na baadhi ya raia kutokana na jinsi yanavyojitokeza.

Kuna shule nyingi ambazo hazikujulikana hasa kutoka kaunti ya Kisii ambazo zimeibuka kuwa juu kabisa na kushinda shule ambazo zinatambulika kama mabingwa wa masomo.

Waziri Machogu sharti afanye mengi zaidi kuimarisha elimu na kudumisha hadhi ya mitihani nchini.

Pia tunaitakia familia ya mwendazake Magoha utulivu wakati huu wa msiba.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Utawala wa Ruto ujenge uwiano si ulipizaji...

Kiangazi: Chemchemi za maji zakauka katika Kaunti ya...

T L