• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
WANDERI KAMAU: Utawala wa Ruto ujenge uwiano si ulipizaji kisasi

WANDERI KAMAU: Utawala wa Ruto ujenge uwiano si ulipizaji kisasi

NA WANDERI KAMAU

UTAWALA wa Kenya Kwanza umekuwa ukijisawiri kama unaomwogopa Mungu.

Kwenye kampeni zao za kuwania urais katika uchaguzi wa Agosti 9 mwaka uliopita, Rais William Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua walijisawiri kama viongozi ambao “wangerejesha Kenya katika njia ya kimaadili” kama atakavyo Mwenyezi Mungu.

Walijisawiri kama Yoshua na Kaleb katika Biblia, ambao hatimaye waliwaongoza Wana wa Israeli katika Kanani—nchi ya ahadi waliyoambiwa na Mwenyezi Mungu walipotoka nchini Misri, nchi ya utumwa.

Vivyo hivyo, Wakenya waliwaona Dkt Ruto na Bw Gachagua kama ‘Yoshua na Kaleb’ wa kisasa—yaani, ndio wangewakomboa kutoka madhila na mateso yote yaliyohusishwa na utawala wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na mshirika wake wa kisiasa, Bw Raila Odinga.

Imani ya Wakenya wengi ilikuwa kwamba hatimaye, Kenya imo mikononi mwa viongozi ambao wanafaa kwa kila namna—wacha Mungu, wachapa kazi, wasio wakabila, wasio ubaguzi wa kidini, mabarobaro, wenye ufasaha mkubwa wa kimatamshi, wanaotoka katika familia za kawaida, waliosoma, wanaotangamana vyema na raia, wasio kisasi na zaidi ya yote, wasema ukweli.

Hiyo ndiyo imekuwa kaulimbiu yao kuu: kusema na kueleza ukweli daima, hata uwe mchungu kiasi gani.

Hata hivyo, ahadi na sifa hizo zinaonekana kubadilika. Viongozi walioapa kutolipiza kisasi sasa wameanza operesheni kali ya ulipizaji kisasi dhidi ya watu walioonekana kutowaunga mkono.

Cha kushtua ni kuwa, wanaonekana kutomwogopa yeyote. Hawababaiki hata kidogo. Wanalenga kote kote. Bila kuogopa kuhusu yale ambayo huenda yakawaandama baadaye. Lengo lao ni moja: kumpa adhabu kali yeyote aliyewapinga ama kuwaingilia kwa vyovyote vile.

Katika ‘operesheni’ hiyo, ni wazi kuwa aliyeongoza harakati za kuwapinga ni Bw Kenyatta, hasa baada ya kubuni ‘handisheki’ baina yake na Bw Odinga. Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i na Katibu wake, Dkt Karanja Kibicho.

Wameapa kuwapa funzo kali. Moja ya hatua hiyo ni kuwapunguzia walinzi wao—sawa na walivyowafanyia walipokuwa serikalini.

Pili, ni kudai kuwa kampuni za viongozi hao—hasa zile za familia ya Bw Kenyatta—zimekuwa zikikwepa kulipa ushuru. Kwa hilo, Rais Ruto na Bw Gachagua wameapa kufanya kila wawezalo kuhakikisha ‘maadui’ wao wamewajibika; wamelipa ushuru kama Wakenya wale wengine.

Ijapokuwa huu ni mwelekeo mzuri, lazima wawili hao wafahamu kuwa kwa kuanza kuwalenga watu waliowahangaisha, wanajiharibia wao wenyewe.

Siasa za kisasi zitaongeza taharuki za kisiasa nchini, na wale watakaoumia ni raia. Kisasi kitaturejesha pale pale tulipokuwa 2007, wakati nchi ilikuwa imegawanyika katika pande mbili.

Kisasi kamwe hakijengi. Ni wakati wa kuwakomboa raia kutokana na madhila ya ugumu wa gharama ya maisha. Je, wakombozi hatimaye wamegeuka wadanganyifu?

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Lengo la Murang’a Seal ni kusaidia vijana kutimiza ndoto...

WANTO WARUI: Waziri Machogu ana kibarua kigumu cha...

T L